Zenj FM

UPDP kutoa mamilioni kwa wanaotaka kuoa Zanzibar

14 September 2025, 11:18 pm

Mgombea urais Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha the United People’s Democratic Party UPDP, Hamad Mohammed Ibrahim, akikabidhi kadi za chama hicho kwa wananchama wapya waliojiunga na chama hicho.

Na Mary Julius.

Mgombea urais Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha the United People’s Democratic Party UPDP, Hamad Mohammed Ibrahim, ameahidi kuwa endapo itapata ridhaa na kuingia madarakani seriakali yake itajenga viwanda vya kusarifu karafuu na mazao mengine ili kuleta ajira kwa wananchi na kukuza uchumi wa Zanzibar.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho uliofanyika katika viwanja vya Garagara, Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi, Ibrahim amesema wamejipanga kuhakikisha asilimia 80 ya karafuu inasindikwa hapa nchini, na asilimia 20 tu ndiyo itakayosafirishwa nje.

Amesema hatua hiyo itaongeza thamani ya mazao , kuongeza ajira kwa vijana na kufanya watu kutoka mataifa mbalimbali kuja kununua bidhaa zilizoongezwa thamani.

Mgombea huyo amesema ili kuwa na umeme wa uhakika na kuendesha viwanda hivyo serikali yake ita jenga vinu viwili vya nyuklia ili kuwa na chanzo cha uhakika cha nishati hiyo muhimu katika maendeleo
ya viwanda .

Sauti ya Mgombea urais Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha the United People’s Democratic Party UPDP, Hamad Mohammed Ibrahim,

Amesema kila kijana mwenye nia ya kuoa atapatiwa milioni mbili kama msaada kutoka chama na serikali ya UPDP na kwa upande wa bi harusi atapewa milioni moja na laki tano, fedha hizi zitakuwa mtaji
wa maisha yao ya ndoa.

Sauti ya Mgombea urais Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha the United People’s Democratic Party UPDP, Hamad Mohammed Ibrahim.

Kwa upande wake , mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama CHA UPDP Twalib Ibrahim Kadege , ametoa wito kwa wagombea wote kuzingatia amani katika kampeni zao, kwani maendeleo hayawezekani kama hakuna amani.