Zenj FM
Zenj FM
1 September 2025, 7:11 pm

Na Mary Julius.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jaji George J. Kazi, amekabidhi rasmi fomu za uteuzi kwa wagombea wa nafasi ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar .
Hafla hiyo imefanyika katika Ofisi za Tume, Maisara, Wilaya ya Mjini Unguja.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa fomu, Mgombea wa Chama cha UDP, Naima Salum Hamad, amesema akichaguliwa ataweka mkazo katika kuboresha maisha ya wanawake, watoto na watu wenye ulemavu.

Kwa upande wake, Mgombea wa Chama cha MAKINI Ameir Hassan Ameir, amesema sera yake kuu ni kuhakikisha kila Mzanzibari aliyezaliwa Zanzibar anapatiwa shilingi laki tano, pamoja na kuweka kima cha chini cha mshahara kuwa shilingi milioni moja na laki tano.
Aidha amesema lengo lake ni kuona Wazanzibari wanakula kile wanachokitaka na siyo kile wanachokipata.
Naye Mgombea wa UPDP Hamad Mohammed Ibrahimu ameahidi kujenga viwanda vikubwa vya kuzalisha umeme kupitia vinu viwili vya nyuklia vitakavyojengwa Unguja na Pemba, ili kuifanya Zanzibar kuwa nchi ya viwanda.

Kwa upande wake, mgombea wa Chama cha ADC Hamad Rashid Mohammed amesema chama chake kitahakikisha Zanzibar inajitegemea kwa chakula, kwa kupunguza utegemezi wa bidhaa za chakula kutoka nje ya nchi.
Aidha, amesisitiza kuwa wakulima na wavuvi wakipewa vifaa vya kisasa, wataweza kulisha familia zao vizuri huku wakipata ziada kwa ajili ya kuuza na kuongeza kipato.
Naye mgombea wa mwisho kuchukua fomu, Shafi Hassan Suleiman kutoka Chama cha Democratic Party (DP), ameahidi kudumisha amani ya nchi, akisema bila amani hakuna maendeleo yoyote yanayoweza kufikiwa. Kipaumbele chake cha kwanza ni ajira kwa vijana na wananchi wote wa Zanzibar, kwa kujenga viwanda vya kusindika mazao ili kuongeza thamani na soko.
Kuhusu kura ya mapema, Suleiman amesema chama chake kinaunga mkono juhudi za serikali kuhakikisha kuwa wapiga kura wenye shughuli siku ya uchaguzi wanapewa fursa ya kupiga kura mapema.
Aidha, amekemea tabiaa ya baadhi ya wagombea kuhamasisha vurugu, akisisitiza kuwa siasa safi ndio msingi wa amani na utulivu.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa zoezi la utoaji wa fomu kwa wagombea , Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jaji George J. Kazi,amesema vyama 17 vimekabidhiwa fomu kwa wakati na kwa utaratibu mzuri.
Aidha Mwenyekiti Jaji Kazi, amesema Vyama vitatu kati ya hivyo vimewasilisha wagombea wanawake, ikiwa ni hatua kubwa kuelekea usawa wa kijinsia katika uongozi.