Zenj FM

Wagombea wa vyama sita wachukua fomu za uteuzi ZEC

30 August 2025, 6:14 pm

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jaji George J. Kazi amemkabidhi fomu ya uteuzi kwa mgombea wa Kiti cha Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoka Chama cha Cha Mapinduzi CCM Dkt. Hussein Ali Mwinyi Hafla hiyo imefanyika katika Afisi za Tume zilizopo Maisara Wilaya ya Mjini Unguja.

Na Mary Julius.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jaji George J. Kazi, amewakabidhi fomu za uteuzi wagombea wa vyama mbalimbali vinavyotarajia kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar mwaka 2025.

Zoezi hilo la uchukuaji fomu za kugombea urais lilianza na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ambaye pia ni mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambaye alikabidhiwa fomu na kisha kuzungumza na wananchi katika viwanja vya Mao Tse Tung, Zanzibar.

Dk. Mwinyi amewataka wagombea wote kufanya kampeni kwa njia ya kistaarabu na kuepuka siasa za chuki.

Dkt. Mwinyi amewahakikishia wananchi kuwa CCM itaendelea kudumisha hali ya utulivu na amani iliyopo nchini wakati wa kampeni, uchaguzi na baada ya uchaguzi.

Aidha, Dkt Mwinyi ametangaza kuwa kampeni za CCM kwa upande wa Zanzibar zitazinduliwa rasmi Septemba 13, na akawataka wanachama wa chama hicho kuwanadi wagombea wao katika ngazi zote ili chama kipate ushindi.

Sauti ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Kwa upande wake, mgombea wa chama cha NLD, Mfaume Khamis Hassan, alipokea fomu yake na kueleza kuwa kipaumbele chake ni kuwaunganisha Wazanzibari endapo atapewa ridhaa ya kuongoza.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jaji George J. Kazi akimkabidhi fomu ya uteuzi kwa mgombea wa Kiti cha Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoka Chama cha Alliance For African Farmers Party, Said Soud Said , Hafla hiyo imefanyika katika Afisi za Tume zilizopo Maisara Wilaya ya Mjini Unguja.

Naye Mgombea wa chama cha AAFP, Said Soud Said, amesema mojawapo ya sera zake ni kuhakikisha zao la bangi linalimwa kisheria kama njia ya kuongeza kipato cha vijana na taifa, akieleza kuwa mataifa mengi duniani tayari yamekuwa yakilitumia zao hilo kuongeza pato la taifa.

Sauti ya Mgombea wa chama cha AAFP, Said Soud Said,

Mgombea wa chama cha CUF, Hamad Masoud Hamad, naye pia amechukua fomu ya kugombea urais wa Zanzibar,akizungumzai sera ya chama hamad amesema chama chake kitaendeleza yale yote mazuri yaliyo fanya na watangulizi.

Sauti ya Mgombea wa chama cha CUF, Hamad Masoud Hamad.

Kwa upande wake, Mgombea wa chama cha TLP, Hussein Juma Salum, amesema chama chake kitaweka kipaumbele katika kudumisha amani, kukuza kilimo, kuongeza mapato ya taifa, kuondoa kikokotoo cha mishahara na kutoa bima ya afya bure kwa wananchi wote.

Sauti ya Mgombea wa chama cha TLP, Hussein Juma Salum,

Naye Mgombea wa chama cha NRA, Khamis Faki Mgau, ameahidi kuboresha mishahara ya walimu na kuhakikisha wanakuwa na maisha bora, pamoja na kupanua kilimo cha zao la mambungo ili liwe miongoni mwa mazao ya kibiashara yanayochangia uchumi wa taifa.

Sauti ya Mgombea wa chama cha NRA, Khamis Faki Mgau.

Zoezi la uchukuaji wa fomu litaendelea siku ya kesho kwa vyama sita kuchukua fomu kikiwemo chama cha Act Wazalendo,, NCCR MAGEUZI,CCK, SAU,ADA TADEA na UMD.