Zenj FM

Wadau wa uchaguzi watia saini maadili ya uchaguzi Zanzibar

24 August 2025, 4:02 pm

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jaji Mstaafu George Joseph Kazi,akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa Kanuni hizo, iliyofanyika katika Ukumbi wa Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud.

Na Mary Julius.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jaji Mstaafu George Joseph Kazi, amezisihi pande zote tatu zinazohusika katika uchaguzi , Serikali, Tume na Vyama vya Siasa kuhakikisha zinatekeleza wajibu wao kama ilivyoainishwa katika Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa mwaka 2025.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa Kanuni hizo, iliyofanyika katika Ukumbi wa Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud ulipo Afisi Kuu ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC, Jaji Kazi amesema maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Jumatano, tnahitaji mshikamano na uwajibikaji wa pamoja.
Aidha Mwenyekiti amesema kanuni hizo zimeandaliwa kwa mujibu wa kifungu cha 65 cha Sheria ya Uchaguzi Na. 4 ya mwaka 2018, kwa mashauriano na wadau mbalimbali, ikiwemo vyama vya siasa, Mrajisi wa Vyama, na mamlaka za serikali.

Sauti ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jaji Mstaafu George Joseph Kazi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Jaji Aziza Iddi Suwed amesema Kanuni hizi zimelenga kuhakikisha usawa kwa wagombea na kwamba uchaguzi unafanyika kwa misingi ya uhuru, haki, usawa na ushirikishwaji wa makundi yote ya kijamii.

Sauti ya Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Jaji Aziza Iddi Suwed.

Akizungumza kwa niaba ya vyama vya siasa, Katibu Mkuu wa Chama Cha Makini Taifa, Ameir Hassan Ameir, amesema kuwa wako tayari kutii maadili hayo na kuyatumia majukwaa ya kampeni kunadi sera zao kwa njia ya amani.

Sauti ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Makini Taifa, Ameir Hassan Ameir.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Organazesheni CCM Zanzibar Omar Ibrahim  akisaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa mwaka 2025.

Nao Baadhi ya washiriki wa hafla hiyo, wakizungumza mara baada ya kutia saini Kanuni hizo za Maadili ya Uchaguzi, wameelezea kufurahishwa kwao na hatua hiyo, na kuahidi kuyatekeleza kikamilifu yale yote waliyoafikiana
Wamesema wapo tayari kushiriki uchaguzi kwa njia ya amani na mshikamano, huku wakiahidi kuwa mstari wa mbele kulinda utulivu wa nchi wakati wote wa kampeni na baada ya uchaguzi.

Sauti ya washiriki.
Matembezi ya amani yalio anzia katika viwanja vya maisara na kumalizikia katika viwanja vya ofisi za Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC.

Awali Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar aliwaongoza washiriki wa hafla hiyo kwenye matembezi ya amani, huku akitoa wito kwa wagombea na wanasiasa kupanga hotuba zao kwa uangalifu ili kuepuka kauli za uchochezi.

Sauti ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Jaji Mstaafu George Joseph Kazi.

Pamoja na kutia saini Kanuni za Maadili pia, Nembo rasmi ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar 2025 ilizinduliwa, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha uchaguzi wa amani na haki.