Zenj FM

Watoto waathirika wakuu wa ukatili Zanzibar

22 August 2025, 5:45 pm

Asha Mahafoudh Mtakwimu kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar akitoa tarifa za takwimu za ukatili na udhalilishaji wa kijinsia kwa mwezi wa Julai 2025.

Na Berema Suleiman.

Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar imesema jumla ya matukio 107 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa kwa mwezi wa Julai 2025 ambapo waathirika walikuwa 107 huku waathirika wengi wakiwa watoto sawa na asilimia 88.8 wakifuatiwa na wanawake asilimia 11.3 na wanaume asilimia 0.9.
Akitoa tarifa za takwimu za ukatili na udhalilishaji wa kijinsia kwa mwezi wa Julai 2025 Mtakwimu Asha Mahfoudh kutoka ofisi ya mtakwimu mkuu wa Serikali Zanzibar divisheni ya jinsia na Ajira amesema idadi ya matukio kwa mwezi yameongezeka kwa asilimia 10.3 kufikia matukio 107 kwa mwezi Julai m2025 ukilinganisha na matukio 97 kwa mwezi wa Juni 2025.
Amesema wilaya ya Magharib A imeripotiwa kuwa na matukio mengi ukilinganisha na wilaya nyengine, matukio 26 sawa na asilimia 24.3 ikufuatia wilaya ya Kati ambapo yameripotiwa matukio 16 sawa na asilimia 15.0.

Sauti ya Mtakwimu Asha Mahfoudh.

Kwa upande wake Sadik Ali Omar kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto amesema miongoni mwa juhudi zinazochukuliwa na idara hiyo ni kutoa elimu katika maeneo mbalimbali ikiwemo skuli,madrasa na hata katika vikundi vya mazoezi ikiwa na lengo kuu la kuhakikisha wanatokomeza vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.

Sauti ya Sadik Ali Omar kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto.

Nae Mkaguzi wa Polisi kutoka Makao Makuu ya Polisi Zanzibar Insepekta Makame Haji Haji amesema ni wajibu wa jamii kuwacha muhali na kuwa na mashirikiano katika kutoa ushahidi mahakamani jambo litasaidia kutokomeza vitendo hivyo.

Pamoja na hayo amewataka wadau na wanaharakati mbalimbali kuendeleza jitihada za kutokomeza vitendo vya ukatili na udhalilishaji visiwani Zanzibar.

Sauti ya Mkaguzi wa Polisi kutoka Makao Makuu ya Polisi Zanzibar Insepekta Makame Haji Haji.