Zenj FM
Zenj FM
10 August 2025, 6:19 am

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC Jaji Joseph Kazi amewakumbusha wasimamizi wa uchaguzi kuwa Mafanikio ya Tume ya Uchaguzi yapo mikononi mwao kwa kuwa wao ni kiungo muhimu kati ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na jamii.
Na Mary Julius.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Jaji George J. Kazi amewataka Wasimamizi wa Uchaguzi kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu, na kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya Wasimamizi wa Uchaguzi kwa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, yanayofanyika katika Ukumbi wa Jaji Mstaafu Mheshimiwa Hamid Mahmoud uliopo katika Afisi Kuu ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Mwenyekiti amesema wasimamizi ni kiungo muhimu kati ya Tume na jamii, hivyo wanapaswa kutambua dhamana kubwa waliyonayo.
Amesema mafunzo hayo yameandaliwa mahsusi kuwawezesha Maafisa wa Wilaya kuelewa kwa kina wajibu wao katika maandalizi na uendeshaji wa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2025.
Aidha, Mwenyekiti amewasisitiza umuhimu wa kuelewa sheria, kanuni, na miongozo ya uchaguzi, kwani ni msingi muhimu wa kusimamia uchaguzi kwa mafanikio.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Thabit Idarous Faina amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mwendelezo wa maandalizi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa octobar 2025.
Aidha, amesema tarehe 18 Agosti 2025, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ZEC itatoa kalenda rasmi ya uchaguzi, itakayobainisha ratiba kamili ya shughuli zote zitakazofanyika kwenye kuelekea Uchaguzi Mkuu.