Zenj FM
Zenj FM
21 July 2025, 6:14 pm

Na Is haka Mohammed.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi INEC imewataka Waratibu na wasimamizi wa Uchaguzi Pemba Kuzingatia Katiba,Sheria, Kanuni na Miongozo iliyotolewa na itakayolewa na Tume katika kutekeleza majukumu yao ya kusimamia uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Wito huo umetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi INEC Jaji Mstaafu Mbarouk Salum Mbarouk wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa Waratibu wa Uchaguzi na Mratibu wa Mafunzo, Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi wa ngazi za Majimbo kanda ya Pemba uko Ukumbi wa Makonyo Wawi Chake Chake.
Ametoa wito kwa Mratibu na Wasimamizi hao wa Uchaguzi kuvishirikisha vyama vyote vya siasa vilivyo na usajili wa kudumu katika hatua mbali mbali, kujiepusha na ushabiki wa kisiasa na kuacha upendeleo wa aina yoyote katika utoaji wa ajira kwa watendaji wa Tume.
Aidha Jaji Mstaafu Mbarouk amewaagiza wasimamizi hao kufanya utambuzi wa vituo vya kupigia kura na mapema na kutoa taarifa kwa wadau, pamoja na kutoa taarifa za kuapishwa kwa mawakala wa vyama vyote kwa wakati na mahala sahihi palipopangwa kufanyika zoezi.
Kaimu Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi INEC Adam Mkina amesema watendaji wa Tume Huru ya Uchaguzi kutekeleza majukumu yao kwa usiri wakizingatia Katiba, Sheria na Kanuni na viapo walivyokula.
Akizungumza mara baada ya kumwapisha Mratibu wa Uchaguzi, Mratibu wa Mafunzo na Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Majimbo Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Nassor Suleiman Nassor amewataka kufuata uadilifu katika kutekeleza majukumu yao.