Zenj FM
Zenj FM
17 July 2025, 5:08 pm

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi akitakta utepe wakati wauzinduzi rasmi Jengo jipya na la kisasa la Afisi Kuu ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) lililopo Maisara, Mkoa wa Mjini Magharibi.Katika kuthamini juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi ,Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imemtunuku Rais huyo Tuzo Maalum kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha demokrasia na mazingira bora ya utendaji wa Tume.
Na Mary Julius
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amezindua rasmi jengo jipya na la kisasa la Afisi Kuu ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), lililopo Maisara, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Uzinduzi huu ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuimarisha mazingira bora ya utendaji kwa taasisi muhimu za demokrasia.
Rais Dkt. Mwinyi amesema ujenzi wa jengo hilo ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, ambapo Serikali ilitumia shilingi bilioni 14.1 kugharamia mradi huo kupitia kampuni ya ujenzi ya CRJE.
Akihutubia kwenye hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali haikusita kufanikisha ujenzi wa makao hayo kwa kutambua nafasi ya ZEC katika kuhakikisha chaguzi huru, haki na za kuaminika.
Rais Dk Mwinyi ameipongeza ZEC kwa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, hasa kwa kusimamia kwa utulivu na ufanisi zoezi la uandikishaji wa wapiga kura. Aidha,amewahimiza wananchi ambao bado hawajachukua vitambulisho vyao vya kupigia kura kuhakikisha wanatimiza haki yao ya kidemokrasia kwa amani.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.Naye Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jaji George J. Kazi, amesema tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, ZEC ilikuwa ikiendesha shughuli zake katika mazingira magumu.
Amesema jengo jipya litaiwezesha Tume kutekeleza majukumu yake kwa weledi zaidi.
Aidha Jaji Kazi amesema ZEC imejipanga kukamilisha maandalizi ya Uchaguzi Mkuu kwa kutoa elimu kwa wapiga kura, kuendesha mikutano ya wadau na mafunzo mbalimbali, huku ikihakikisha kila mwenye sifa ya kupiga kura anapata nafasi hiyo kwa haki.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Thabit Idarous Faina amesema kukamilika kwa jengo hilo kunadhihirisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Nane katika kuimarisha utawala bora, uwazi na ufanisi wa chaguzi.