Zenj FM
Zenj FM
5 July 2025, 9:05 pm

Serikali ya Mapinuzi ya Zanzibar imejipanga kufanya mageuzi kwenye Sekta ya Ushirika ili kuhakikisha inavijenga Vyama vya Ushirika kuwa imara, endelevu na vyenye kutoa tija kwa Wanachama wake.
Na Mary Julius.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema imedhamiria kuendeleza juhudi za kuimarisha miundombinu bora ya biashara na uwekezaji ili kuiwezesha sekta ya ushirika kushamiri na kuchangia kikamilifu maendeleo ya kiuchumi ya nchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, ameyasema hayo alipomuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, katika maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja.
Hemed amesema ipo haja ya kufanya mageuzi ya kina kwenye vyama vya ushirika ili kuviwezesha kwenda kisasa na kuongeza uwezo wao wa kushiriki ipasavyo katika uchumi wa Zanzibar.
Aidha amesema serikali imefanikiwa kuviunganisha vyama 383 vya uzalishaji na vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) Unguja na Pemba, hatua iliyoleta tija kwa kuwapatia mitaji wanachama wake.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi, Uchumi na Uwekezaji), Shariff Ali Shariff, amesema Katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza ya Awamu ya nane mafanikio makubwa yamepatikana ikiwemo kuimarika kwa Uchumi wa Vyama vya Ushirika vya Kilimo, Uvuvi, Ufugaji, Kazi za mikono, Utalii, Viwanda vidogo na Biashara.
Aidha Waziri Shariff amesema Serikali imefanikiwa kutoa mafunzo ya uendeshaji na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika kwa Vyama 6,801 Unguja na Pemba vyenye Wanachama 40,762 wanawake 27,070 na wanaume 13,692). Pamoja na kutatua migogoro mikubwa 40 kwenye Vyama vya Ushirika Unguja na Pemba.
Naye Katibu wa vyama vya ushirika Zanzibar, Suleiman Ali Haji, akisomrisala ya wanaushirika, amesema vyama hivyo vinaendelea kuwa chachu ya kutatua changamoto za kiuchumi na kuongeza kipato kwa wananchi, hususan vijana na wanawake kupitia ajira na mikopo.
Aidha suleiman amesema Wanaushirika wa Zanzibar wanawapongeza Maraisi wote wawili, Raisi wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Dr Samia Suluhu Hassan na Raisi wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr Hussein Ali Mwinyi kwa kusimamia miradi ya maendeleo ambayo imeleta neema kwa Wazanzibari na kuchangia kukua kwa uchumi wa Zanzibar.
Katika hafla hiyo Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Suleiman Abdulla amezindua ushirika online tv.