Zenj FM
Zenj FM
2 July 2025, 6:57 pm

Na Ivan Mapunda.
Takwimu zinaonesha bado hakuna uwakilishi wa kutosha wa wanawake katika nafasi za uongozi, za kuchaguliwa au kuteuliwa katika ngazi mbalimbali za uongozi na hata hivyo ukilinganisha na tulipotoka, kuna mabadiliko chanya katika ushiriki wa wanawake na uongozi.
Lengo namba 5 la Malengo ya Maendeleo Endelevu linataka wanawake washiriki kikamilifu na kwa tija na fursa sawa katika uongozi na ngazi zote za maamuzi katika siasa, uchumi na Maisha kwa ujumla.
hali ilivyo sasa tofauti na zamani
Kuna wanawake wengi zaidi ambao wamepiga hatua na kufanikiwa kuendesha njia yao katika eneo lililotawaliwa zaidi na wanaume.
Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa kama Rais wa Tanzania akikanyaga viatu vya mtangulizi wake John Pombe Magufuli aliyefariki dunia akiwa madarakani. Na sio mbali sana, Kusini, Netumbo Nandi-ndaitwah: hivi karibuni alichaguliwa kuwa Rais wa kwanza mwanamke wa Namibia, na kupata asilimia 57 ya kura.
Rwanda, ambayo mara nyingi inasifiwa kwa sera zake za kimaendeleo, ina asilimia 61.3 ya wanawake bungeni, kielelezo cha ushirikishwaji na usawa.
Katika bara la nchi 54, kwa nini ni nchi chache zinazoongozwa na wanawake
Vikwazo Vya Kitamaduni na Dini
Tamaduni nyingi barani Afrika bado zinaamini kuwa wanawake hawapaswi kuwaongoza wanaume.
Tunu Juma Kondo Naibu Katibu Mkuu Umoja wa Wanawake UWT anayefanyia kazi zake Zanzibar amesema mila kandamizi, desturi na mitizamo hasi dhidi ya ushiriki wa wanawake katika maamuzi pamoja kuwepo kwa changamoto ya ukosefu wa mifumo rasmi na wezeshi ya Kikatiba, na Kisheria katika usawa wa nafasi za uongozi.
” Amesema kwa sasa kuna unafuu ikilinganishwa na tulipotoka kuna mabadiliko chanya katika ushiriki wa wanawake katika uongozi zamani wanawake wengi walikua wanaogopa kujitokeza katika nafasi mbali mbali za uongozi kwa sababu ya mfumo dume ulikua umetutawala na mwanamke alikua anaonekana haweazi kuongoza”
”Sasa Ni Wakati Muafaka Wanawake Wenyesifa kujitokeza kwa wingi kwenda majimboni kuogombea nafasi sawa na wanaume ili kuongeza idadi ya wanawake katika ngazi za maamuzi na kushika nafasi hizo huku akiomba jamii hususani wanaume kuondoa dhana potofu na hivyo kutoa nafasi kwa wake zao kugombea nafasi za uongozi. ”
Ameongeza kuwa pamoja na kuwepo kwa viongozi wanawake katika nafasi za juu lakini bado hakuna uwakilishi wa kutosha wa wanawake katika nafasi za uongozi za kuchaguliwa na kuteuliwa katika ngazi mbalimbali za uongozi .
Pavu Abdallah kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja Naibu Katibu wa Haki za Binadamu na Vyombo vya Wakilishi Wananchi ACT wazalendo amesem kuwa bado hakuna mifumo rasmi na wezeshi ya kikatiba , kisheria na kisera, katika usawa katika nafasi za uongozi. Mila kandamizi, desturi na mitizamo hasi dhidi ya ushiriki wa wanawake katika maamuzi bado ni changamoto kubwa katika jamii yetu.
Ripoti ya TAMWA-Zanzibar inaonesha kuwa katika uchaguzi wa 2020, wanawake waliopata nafasi ya uwakilishi katika majimbo ya Zanzibar walikuwa nane tu kati ya 50.
Wabunge wanawake waliowakilisha Zanzibar walikuwa wanne, mawaziri sita (asilimia 33), makatibu wakuu saba (asilimia 39), huku mkuu wa mkoa mmoja tu akiwa mwanamke.
Wakuu wa wilaya walikuwa wanne, wakifikia asilimia 36, na masheha wanawake walikuwa 68 kati ya 389, sawa na asilimia 17.
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA- Zanzibar Dkt,Mzuri Issa amesema wanawake mbali na changamoto ya umasikini wafedha ila bado wanapitia changamoto kubwa ya ukatili wa kijinsia.
”wanawake wanapamba na vitendo vikubwa vya ukatili ndani ya chama na nje ya chama tulishuhudia uchaguzi wa mwaka 2020 ulikua na vurugu ambapo wanawake waliathirika zaidi na nguvu zilitumika dhidi ya wanawake na kupelekea hofu kwao ya kushiriki katika nafasi za uongozi. ”
” Hili ni jambo kubwa kama nchi inapaswa kulishughulikia ili wanawake wakapata nafasi zaidi ya kushiriki katika nafasi za madaraka”
Mikakati ya kufanikiwa
Sheria ya vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992 inahimiza usawa wa kijinsia katika utekelezaji wa sera za vyama.
Hata hivyo, utafiti wa mwaka 2013 uliobaini kuwa vyama vingi bado havijaweka mazingira mazuri kwa wagombea wanawake, unathibitisha kuwa utekelezaji wa sheria hiyo unakumbwa na changamoto.
Juma Ali Khatib Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania anakiri kuwepo kwa changamoto za kijinsia lakini anasisitiza kuwa baraza la vyama la siasa inatekeleza sera jumuishi inayolenga kuhamasisha ushiriki wa jinsia zote katika siasa.
”Mimi kama mwenyekiti wa baraza la vyama vya siasa tanzania tuliwaommba mtandao wa jinsia tanzania- TGNP, kutupa mafunzo elekezi ya kuingiza katika katiba zetu za vyama vya siasa kila chama iwe na kipengele kinachoeleza wazi jinsi ya ushirikishwaji wawanawake ”amesema
Pamoja na vikwazo vya kijamii na kisiasa, wanawake wanapaswa kuendelea kujiamini na kushirikiana kuleta mabadiliko.
uhamasishaji na kuwawezesha wanawake kiuchumi ni hatua muhimu katika kufanikisha ajenda ya usawa wa kijinsia.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,anasema Chama Cha Mapinduzi na viongozi wakuu wanaendelea kutoa nafasi kwa wanawake na wanafanya vizuri.
”Wanawake wamepewa nafasi kubwa sana katika chama cha mapinduzi na kimeendelea kuwaamini na kuwaanda kuwa viongozi. ”
”Ili kutengeneza nafasi kwa wingi na kuongeza idadi ya wanawake katika uongozi sasa umefika wakati wa wanawake kuachilia viti maalum na kwenda kugombania sawa na wanaume ”.
Ismail Jussa Ladhu Makamo Mwenyekiti wa Chama Cha ACT Wazalendo amesema sera ya jinsia katika chama chao imeanza kutekelezwa kwa kishindo na vitendo na kupelekea wanawake kupata nafasi sawa na wanaume.
Sera yetu ya jinsia inasema katika uongozi wa taifa angalau kuwe na asilimia 30 katika Uongozi wa chama cha act wazalendo unaviongozi saba katika saba wawili ni wanawake ambao sawa na asilimia 29 hivyo tumekalibia asilimia 30.jussa anasema
Mkurugenzi Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar Zafela Jamila Mahamoud Juma anasema pamoja na kujivunia kuwa na wanawake viongozi katika nafazi za juu za maamuzi katika mihimili miwili (Serikali na bunge) pamoja na maeneo mengine, bado kuna changamoto kubwa katika kufikia 50/50.
Ameeleza kuwa bado hakuna mifumo rasmi na wezeshi ya kikatiba , kisheria na kisera, katika usawa katika nafasi za uongozi.
“Kwa wale waliofanikiwa kuwa viongozi walau katika nafasi ndogo za maamuzi, wamekuwa wakiacha nafasi hizo kutokana na kukosekana kwa mfumo wa kuungwa mkono (supportive mechanism) kuanzia kwenye ngazi ya familia hadi jamii kwa ujumla”. Amesema
“Tunaendelea kutoa elimu kwa njia mbalimbali katika kuhakikisha wanawake wanatambua uwezo wao, fursa na namna wanavyoweza kubadili sura ya mfumo kandamizi,” anasema.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini mikataba mbalimbali ya kimataifa kama mkataba wa CEDAW ulioanzishwa mwaka 1979 ukiwa na lengo la kupinga aina zote za udhalilishaji dhidi ya wanawake,itifaki ya SADC ya mwaka 2008 na itifaki ya Maputo ya mwaka 2003