Zenj FM
Zenj FM
20 June 2025, 3:48 pm

“katika kuendeleza juhudi za kusaidia jamii katika kupambana na urahibu wa madawa ya kulevya, Mamlaka imetangaza nafasi kumi (10) kwa vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35 ambao wameamua kwa hiari kuachana na matumizi ya madawa ya kulevya kwa kuwapatia matibabu bure na mafunzo ya ujasirimali”
Na Mary Julius
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar imetaifisha nyumba yenye thamani ya Shilingi milioni 969 inayodaiwa kuwa mali ya Said Seif Salum, anayetuhumiwa kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya visiwani humo.Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar, Kanal Burhan Zubeir Nassor, amesema hatua hiyo imekuja baada ya kukamatwa kwa watu wawili wanaodaiwa kuwa wafanyakazi wa karibu wa mtuhumiwa huyo ambao ni Ali Mohammed Ali, maarufu kama Ali Macho, na Fahad Ali Khamis, ambao walikamatwa wakiwa na gramu 200 za dawa ya kulevya aina ya Cocaine.
Kanal Burhan, amesema Said Seif Salum anatajwa kuwa miongoni mwa vinara wa mtandao wa kimataifa wa usafirishaji na usambazaji wa dawa za kulevya katika Ukanda wa Afrika Mashariki, ambapo inadaiwa kuwa amekuwa akihusika kuingiza dawa hizo kutoka Afghanistan na kuzisambaza katika nchi mbalimbali za ukanda wa afrika mashariki.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar imetangaza zawadi ya Shilingi milioni 10 kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kufanikisha kukamatwa kwake au kugundua mali nyingine zinazomilikiwa naye.
Aidha katika kuendeleza juhudi za kusaidia jamii katika kupambana na urahibu wa madawa ya kulevya, Mamlaka imetangaza nafasi kumi (10) kwa vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35 ambao wameamua kwa hiari kuachana na matumizi ya madawa ya kulevya kwa kuwapatia matibabu bure na mafunzo ya ujasirimali.