Zenj FM
Zenj FM
19 June 2025, 3:14 pm

“Maonyesho haya yamelenga kuitangaza Zanzibar na Tanzania kama kivutio kikuu cha utalii barani Afrika Lengo likiwa ni kuyafanya maonyesho hayo kuwa ya kiwango cha juu”
Na Mary Julius
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mudrick Ramadhan Soraga amesema zaidi ya watu mia saba (700) wanatarajiwa kushiriki katika ufunguzi wa Maonyesho ya Utalii na Uwekezaji yanayotarajiwa kufanyika katika viwanja vya Nyamanzi, Zanzibar kuanzia tarehe 20 hadi 21 Juni 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ukaguzi wa maandalizi ya maonyesho hayo, Waziri soraga amesema maandalizi kwa ajili ya maonyesho hayo ambayo ni ya pili kufanyika visiwani Zanzibar yamekamilika kwa asilimia kubwa.
Waziri Soraga amesema Maonyesho haya yamelenga kuitangaza Zanzibar na Tanzania kama kivutio kikuu cha utalii barani Afrika Lengo likiwa ni kuyafanya maonyesho hayo kuwa ya kiwango cha juu .
Waziri Soraga amesema , tuzo mbalimbali zitatolewa kwa watu na taasisi zilizotoa mchango mkubwa katika kukuza sekta ya utalii nchini, miongoni mwa watakaotunukiwa tuzo hizo ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa mchango wao mkubwa katika kutangaza utalii wa Tanzania kimataifa.
Aidha Waziri amesema Maonyesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kukuza ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi katika kuimarisha uwekezaji kwenye sekta ya utalii na kutoa fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.