Zenj FM

Ucheleweshaji wa leseni kuwa historia, Serikali yaja na mfumo wa haraka

17 June 2025, 1:24 pm

Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Nadir Abdul-latif Yussuf.

Na Mary Julius.

Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Nadir Abdul-latif Yussuf, amesema Mamlaka ya Leseni na Usalama Barabarani imekamilisha maandalizi ya mfumo mpya wa kidijitali utakaoimarisha utoaji wa matokeo ya majaribio ya udereva ndani ya muda mfupi.
Amesema hayo kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo alipokuwa akijibu swali la Mwakilishi Chumu Kombo Khamis (nafasi za wanawake), ambaye alitaka kujua sababu za ucheleweshaji wa hati za udereva kwa wahitimu wa mafunzo.
Naibu Waziri amesema kwa sasa ucheleweshaji huo unasababishwa na utaratibu wa sasa ambapo wapasishaji huwafanyia madereva majaribio na kisha kuandaa matokeo kwa ajili ya kuwasilishwa, ili nambari za siri za leseni zitengenezwe, Mchakato huo unachukua muda hadi wiki moja au zaidi.
Naibu Waziri, amesema mfumo mpya uliotengenezwa utawezesha madereva wanafunzi kupata matokeo yao ndani ya nusu saa tu baada ya kufanya majaribio, hatua itakayopunguza kwa kiasi kikubwa ucheleweshaji wa utoaji wa leseni.
Aidha Naibu waziri amesema Mfumo huo unatarajiwa kuanza kutumika rasmi kuanzia mwezi Julai mwaka 2025.

Sauti ya Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Nadir Abdul-latif Yussuf.