Zenj FM

ZEC mguu sawa uchaguzi 2025, ofisi mpya yazinduliwa Magharibi B

10 June 2025, 3:21 pm

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jaji George J. Kazi akiwa na Makamo Mwenyekiti Jaji Aziza Suwed wakiweka jiwe la msingi katika eneo la Mazizini, Unguja, ambako ofisi hiyo mpya inajengwa.

Na Mary Julius.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jaji George J. Kazi , amesema ujenzi wa ofisi ya Tume ya Uchaguzi katika Wilaya ya Magharibi B utasaidia kusogeza huduma karibu na wananchi wa eneo hilo.

Mwenyekiti George ameyasema hayo wakati akiweka jiwe la msingi katika eneo la Mazizini, Unguja, ambako ofisi hiyo mpya inajengwa Mwenyekiti amesema kuwa hapo awali, Tume ilikuwa ikitumia ofisi za Wilaya ya Magharibi A kutoa huduma zake, hivyo ujenzi huu ni hatua muhimu katika kuhakikisha huduma za Tume zinapatikana kwa urahisi na kwa wakati kwa wananchi wa Wilaya ya Magharibi B.

Mwenyekiti amesema hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya Tume ya kuboresha utendaji kazi wake, kwa kuhakikisha uwepo wa vitendea kazi vya kutosha pamoja na miundombinu bora ya ofisi, hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Aidha, Mwenyekiti amesema Tume inatarajia kuanzisha ofisi nyingine katika wilaya mbalimbali za Unguja na Pemba, ili kuongeza ufanisi katika kutoa huduma kwa wananchi wote wa Zanzibar.

Sauti ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jaji George J. Kazi.

Naye, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC Thabit Idarusi Faina , amesema Tume ya Uchaguzi Zanzibar ina jumla ya ofisi 11 katika wilaya zote za Unguja na Pemba, na kukamilika kwa ujenzi huu kutaimarisha zaidi uwezo wa Tume katika kutoa huduma bora na kwa ufanisi.

Sauti ya Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC Thabit Idarusi Faina.

Kwa upande wake, Mshauri Elekezi kutoka wakala wa Majengo Zanzibar Arafa Haji Ali amesema hadi sasa ujenzi wa ofisi hiyo umefikia asilimia 80, huku gharama za ujenzi zikifikia shilingi milioni 315.

Aidha amesema majengo hayo yamezingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu ili kuhakikisha huduma jumuishi kwa wananchi wote.

Sauti ya Mshauri Elekezi kutoka wakala wa Majengo Zanzibar Arafa Haji Ali.