Zenj FM
Zenj FM
29 May 2025, 7:23 pm

Na Mary Julius.
Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Tawala za Mikoa, Zainab Khamis Kibwana, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuziangalia taasisi za serikali za mitaa kama nguzo muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo kitaifa.
Mkurugenzi ameyasema hayo wakati wa akifunga mafunzo ya siku nne kwa Maafisa Mapato na Wahasibu kutoka mabaraza ya manispaa, yaliyoandaliwa na mradi wa ukuaji uchumi jumuishi Zanzibar (BIG Z) kwa ushirikiano na Benki ya Dunia, mkoa wa mMjini Magharib Unguja .
Amesema endapo taasisi hizo zitashindwa kusimamia vyema majukumu yao, mzigo mkubwa utabaki kwa serikali kuu, hali inayoweza kudhoofisha juhudi za utekelezaji wa mipango ya kitaifa na maendeleo ya nchi.
Aidha Zainab amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha wanatumia maarifa waliyoyapata kuimarisha utendaji kazi katika ukusanyaji wa mapato, kusimamia rasilimali kwa uadilifu, na kubuni vyanzo vipya vya mapato vinavyoweza kusaidia taasisi zao kuwa imara kifedha.
Kwa upande wake Mtaalamu wa Mipango Miji na Mfumo wa Jiografia, Deogratias Evarist Minja, amesema ushirikiano kati ya Benki ya Dunia na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika utekelezaji wa mradi wa BIGZ, una lengo la kuwajengea uwezo watumishi wa serikali za mitaa ili kuboresha ufanisi na utendaji wa kila siku wa taasisi zinazohusika katika huduma za umma.
Aidha Minja amesema mafunzo haya ni hatua muhimu itakayochangia mabadiliko katika usimamizi na utoaji wa huduma katika serikali Zanzibar.
Kwa upande wao washiriki wa mafunzo wameahidi watayatumia katika kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza mapato katika taasisi zao.