Zenj FM
Zenj FM
28 May 2025, 4:47 pm

Na Mary Julius.
Jamii imetakiwa kuachana na imani potofu zinazohusiana na watu wanaopungukiwa damu mara kwa mara kwa kudhani kuwa wamerogwa au wana majini, na badala yake kuwahisha hospitalini ili kupata uchunguzi wa kitabibu.
Akizungumza na Zenji FM, ikiwa ni maadhimisho ya siku ya saratani ya damu,Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani Zanzibar Dk Hellen Makwani amesema kumekuwa na mtazamo usio sahihi kwa baadhi ya watu kudhani kuwa ndugu zao wanaoumwa mara kwa mara na kupungukiwa damu wananyonywa damu na majini, hali ambayo imekuwa ikiwafanya kuacha kufuata matibabu sahihi ya hospitali na badala yake kukimbilia kwa waganga wa kienyeji.
Dkt. Hellen ameeleza kuwa kupungukiwa damu mara kwa mara kunaweza kuwa dalili ya magonjwa mbalimbali ya ndani, ikiwa ni pamoja na saratani ya damu (leukemia).
Aidha Dkt. Hellen amesema wazazi na walezi wanapaswa kuwajengea watoto wao utaratibu wa kufanya mazoezi na kazi ndogo ndogo ili kujenga kizazi kinacho jishughulisha na kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza.
Nao baadhi ya Wazazi wamesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejenga viwanja vingi vya michezo, hivyo ni wajibu wa wazazi kuvitumia viwanja hivyo kwa manufaa yao na ya vizazi vijavyo, ili kuepuka tabia ya uzembe na bwete miongoni mwa vijana.
Kila ifikapo Mei 28, dunia huadhimisha Siku ya Saratani ya Damu kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa huo na kuhimiza upatikanaji wa huduma bora kwa wagonjwa.