Zenj FM
Zenj FM
19 May 2025, 5:03 pm

Na Mary Julius.
Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said, ameitaka Tume ya Mipango Zanzibar kuandaa waraka mahsusi utakaoelezea kwa kina namna ya utekelezaji wa mfumo wa ukusanyaji, uhifadhi, na usambazaji wa taarifa za kijiografia , ili kuwasilishwa katika taasisi husika kwa ajili ya utekelezaji.
Akizungumza katika semina ya watendaji wakuu wa Serikali juu ya utekelezaji wa mfumo huo iliyofanyika huko Verde, Mhandisi Zena amesema mfumo huo ulianzishwa muda mrefu uliopita lakini ulipata changamoto za kiutendaji ambazo zilisababisha kushindwa kufanya kazi kama ilivyokusudiwa.
Aidha ameipongeza Tume ya Mipango Zanzibar kwa kuamua kuandaa mfumo huo ambao utasaidia katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendelea nchini.
Akimkaribisha mgeni rasmi , Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar, Dkt. Rahma Salim amesema ili kufanikisha dira ya maendeleo ya Zanzibar Vision 2050, kutimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), na kufikia malengo ya Ajenda ya Afrika 2063, Zanzibar inahitaji kuwa na mfumo imara unaowezesha ukusanyaji na matumizi ya takwimu sahihi za kijiografia.
Aidha amesema matumizi ya data sahihi na za wakati yatasaidia katika kurahisisha ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, kusimamia vyema matumizi ya ardhi, na kusaidia upangaji wa miji kwa kuzingatia mahitaji halisi ya jamii.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar, Dkt. Rahma Salim.Kwa upande wake Afisa Tehema Kamisheni ya Ardhi Ibrahim Khalid Mambo amesema moja ya sababu za mfumo huo kutofanya kazi awali ilikuwa ni ukosefu wa mashirikiano ya pamoja kati ya taasisi mbalimbali.
Nae Kaimu Mratibu wa Mradi wa BIG-Z Hamad Bakari amesema Mradi wa Kuongeza Ukuaji Endelevu Zanzibar (BIG-Z), unaofadhiliwa na Benki ya Dunia,umelenga kukuza uchumi wa Zanzibar kupitia maendeleo ya miundombinu, utalii endelevu, na kuboresha maisha ya jamii katika maeneo ya Chwaka, Makunduchi, na Nungwi kwa upande wa Pemba mradi unatekelezwa Chakechake, Wete, Mkoani na Micheweni.