Zenj FM
Zenj FM
13 May 2025, 2:25 pm

Mary Julius.
Kadhi wa Wilaya ya Kusini Abubakar Ali Mohamed amesema utekelezaji wa Kampeni ya msaada wa kisheria katika kutoa elimu kwa wananchi hasa wa vijijini kumesaidia wananchi wengi kuzitambua njia na taratibu za kisheria katika kudai haki zao zinazohusiana na masuala ya ndoa, mirathi wasia na masuala mengine yanayohusiana na jamii.
Ameyasema hayo huko Skuli ya Paje na kitogani wakati akizungumza na Wananchi hao ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa Kampeni ya msaada wa Kisheria ya mama Samia Legal Aid.
Amesema imeonekana wananchi wengi wamekuwa wakipoteza haki zao kutokana na ukosefu wa elimu na kutokutambua taratibu husika juu ya kupata haki zao hivyo wana matarajio baada ya kukamilika kwa mpango huu jamii itakuwa na mwamko wa kufuata taratibu na sheria katika kudai haki zao katika vyombo vinavyohusika.
Kwa upande wake Afisa Usajili wa matukio ya kijamii Wilaya ya Kusini Abdulhamid Khamis Kombo amesema ipo haja kwa taasisi yake kuongeza juhudi zaid ya utoaji wa elimu kwa wananchi hasa wa vijijini ili kuona kila mwananchi anaestahiki na anasifa ya kupata vitambulisho anapatiwa haki hiyo tena kwa wakati.
Nao baadhi ya wananchi shehia hizo waliofika kupatiwa Elimu hiyo wamezishukuru serikali zote mbili kuja kwa mpango huo kwani utasaidia kuondosha changamoto za kisheria zinazowakabili iwapo maoni, ushauri na maelekezo ya wananchi yatafanyiwa kazi na mamlaka zilizohusishwa katika Kampeni hii ya msaada wa kisheria zitayafanyia kazi.