Zenj FM

Mwenyekiti UWZ atoa wito wa mshikamano

12 May 2025, 12:55 pm

Mwenyekiti wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, UWZ Abdulwakili H Hafidhi, akiwa p[omoja na baadhi ya viongozi wapya wa umoja huo wilaya ya Kaskazini B katika skuli ya Mahonda.

Na Mary Julius.

Mwenyekiti wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, UWZ Abdulwakili H Hafidhi, amewataka wanachama wa umoja huo kuunga mkono viongozi wao kwa lengo la kuhakikisha kuwa huduma na mafanikio ya umoja huo yanawafikia watu wote wenye ulemavu visiwani Zanzibar.
Akizungumza katika ziara ya kutambulisha uongozi mpya wa umoja huo kwa wanachama wa Mkoa wa Kaskazini, Abdulwakili amesema ushirikiano wa pamoja baina ya wanachama na uongozi ni njia muhimu ya kutatua changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu na kuongeza mafanikio ya umoja huo.
Aidha amesema mshikamano na mawasiliano ya karibu vitasaidia kujenga taasisi imara inayojali ustawi wa wanachama wake na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Sauti ya Mwenyekiti wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, UWZ Abdulwakili H Hafidhi.
Baadhi ya wanachama wa Umoja wa Watu wenye Ulemavu UWZ wa Wilaya ya Kaskazini A.

Wakizungumza na uongozi mpya wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar UWZ , baadhi ya wanachama wamewaomba viongozi hao kuendeleza mshikamano na kutimiza ahadi wanazotoa kwa wanachama, ili kujenga uaminifu na kuimarisha ushirikiano.
Wanachama hao pia wamewataka viongozi wao kuendelea kuwasimamia kwa karibu na kuwatetea katika nyanja mbalimbali, ili kuhakikisha wanapata haki zao na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.
Wanachama hao wamewashukuru viongozi kwa jitihada zao za kuwafika katika maeneo yao, hatua ambayo ni ishara ya kujali na dhamira ya kweli ya kuwatumikia watu wenye ulemavu.

Sauti ya wanachama wa UWZ mkoa wa kaskazini unguja.

Katika ziara hiyo Mwenyekiti Abdulwakili aliongozana na viongozi wa juu wa umoja huo ambapo wametembelea wilaya mbili zilizopo katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.