Zenj FM

Hatimaye Mv mapinduzi II yakaribia kurudi kazini

2 May 2025, 2:29 pm

Meli ya MV MAPINDUZI (II) ikiwa katika safari ya majaribio kuelekea usawa wa Funguni Mashariki mwa Kisiwa cha Bawe.

Na Kassim Salum Abdi.

Kamati ya kudumu ya Baraza la Wawakilishi inayosimamia Mawasiliano, Ardhi na Nishati imesema imeridhishwa na matengenezo ya ukarabati wa Meli ya MV MAPINDUZI (II) iliopo nangani katika bandari ya Malindi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati Yahya Rashid Abdalla ameeleza hayo wakati walipokuwa katika majaribio ya kuitembeza meli hiyo kutoka katika bandari ya Malindi kuelekea usawa wa Funguni Mashariki mwa Kisiwa cha Bawe.
Yahya ameeleza kuwa, meli hiyo kwa sasa inatembea vizuri ambapo ameupongeza uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kupitia Shirika la Meli Zanzibar kwa usimamizi makini katika kuhakikisha matengenezo ya awali yanakamilika.

Aidha, Mwenyekiti huyo amelishauri Shirika la Meli kupitia Mkurugenzi Muendeshaji kuendelea kusimamia kwa karibu kukamilika kwa matengenezo ya mwisho ili Meli ya MV MAPINDUZI (II) Ianze kutoa huduma zake kama kawaida kwa wananchi.

Nae Mkurugenzi Muendeshaji wa Shirika la meli Zanzibar Mhandisi Makame Hasnuu Makame (Chief) ameipongeza Kamati hiyo kwa maelekezo na miongozo yake kwa shirika jambo linalosaidia kufikia mafanikio ya Shirika hilo.

Mkurugenzi Hasnuu ameihakikishia Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati kwamba, Shirika halitarudi nyuma na litafanya kila aina ya uwezekano ili kukamilisha matengenezo ya meli ya MV MAPINDUZI (II) na muda wowote kutoka sasa meli itapelekwa chelezoni Mombasa kwa ajili ya kukamilishwa kwa matengenezo ya mwisho.