Zenj FM
Zenj FM
30 April 2025, 3:59 pm

Na Mary Julius.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema Serikali ya Awamu ya sita inaendelea na utekelezaji wa miradi ambayo ni wezeshi katika sekta ya Uchukuzi inayojumuisha ujenzi wa reli ya kisasa, ukarabati wa viwanja vya ndege na vivuko kwa lengo la kuunganisha huduma na miundombinu ya Uchukuzi.
Ameyasema hayo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanznaia, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika ufunguzi Mkutano wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mawakala wa Ushuru na Forodha kwa Kanda ya Afrika na Mashariki ya Kati wa mwaka 2025, uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip.
Serikali inaendelea kuchukua hatua mbali mbali ikiwemo kuboresha mifumo, kujenga na kukarabati miundombinu, kushirikisha Sekta binafsi katika uendeshaji wa shughuli za bandari na kutoa elimu binafsi katika uendeshaji wa shughuli za bandari.
Amesema Shirikisho la Vyama vya Mawakala wa Ushuru na Forodha, limekuwa likifanya kazi kubwa ikiwemo kuandaa mikutano na kusaidia vyama vya Mawakala wa Ushuru na Forodha Duniani katika kutimiza majukumu yao kwa mujibu wa Mikataba, Sera na Sheria za Kimataifa.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, zitaendelea kuthamini mchango unaotolewa na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mawakala wa Ushuru na Forodha kwa Kanda ya Afrika na Mashariki ya Kati.
Kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imefanya maboresho makubwa kwenye sekta ya Uchukuzi na kuweza kupata mafanikio chanya ambayo yameleta mabadiliko makubwa katika utoaji wahuduma.
Akimkaribisha mgeni rasmi Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema ushirikiano uliwekwa na serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na wadau wa sekta ya uchukuzi umewezesha kuendelea kukua kwa mizigo inayo pitia nchini kuelekea nchi za jirani.
Aidha waziri amesema maboresho na ushirikihwaji wa sekta binafsi katika bandari ya dar es salama umeongeza mapato yanayotokana na shughuli za bandari.
Nae Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Mawakala wa Ushuru na Forodha (Fiata), Turgut Erkeskin amesema hatua zinazochukuliwa na Tanzania kuimarisha bandari na ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR, inaboresha uchukuzi na kusaidia maendeleo sio ya Nchi hiyo pekee bali mataifa mengine jirani.
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Makala wa Ushuru na Forodha Tanzania, Edward Urio, amesema kuna mabadiliko makubwa katika sekta ya usafirishaji ikiwemo mageuzi katika Bandari ya Dar es Salaam, uboreshaji wa Bandari kwa kutumia vifaa vya kidijitali ambavyo vinaiwezesha Tanzania kuwa ni miongoni mwa nchi zilizopiga hatua katika hiyo.