Zenj FM

Makarani uandikishaji kisiwani Pemba watakiwa kushirikiana na wananchi

30 January 2025, 2:12 pm

Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Thabit Idarous Faina akizungumza katika mafunzo kwa watendaji wa uandikishaji wa wapiga kura awamu ya pili yaliyofanyika skuli ya Sekondari Madungu.

Na Mary Julius.

Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Thabit Idarous Faina amewataka makarani wa uandikishaji kisiwani Pemba kuwa na ushirikiano na wananchi wanaofika vituoni kuandikishwa sambamba na kutumia lugha fasaha.
Mkurugenzi ameyasema hayo katika mafunzo kwa watendaji wa uandikishaji wa wapiga kura awamu ya pili yaliyofanyika skuli ya Sekondari Madungu, amesema ni vyema kwa watendaji hao kutekeleza majukumu yao kwa uweledi na ufanisi kwa kuzingatia maelezo, miongozo, kanuni na sheria waliyopewa na Tume ya uchaguzi.
Aidha amesema watendaji hao wanatakiwa kuelewa kuwa kazi watakayoifanya vituoni ni jukumu la Kitaifa linalohitaji kuendeshwa kwa uweledi na ustadi ili kupata wapiga kura watakaoamuwa hatima yao ya Demokrasia ya Taifa katika uchaguzi unaofanyika Zanzibar na Tanzania.

Sauti ya Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Thabit Idarous Faina.

Mapema Mratibu Ofisi ya Tume ya uchaguzi Pemba Ali Said Ali amesema mafunzo hayo yatalenga kuwajengea uwezo katika utendaji wa kazi zao hivyo ni vyema kuwa makini ili kuweza kuleta mafanikio yaliyokusudiwa.
Nao Makarani hao wamesema watahakikisha wanafuata taratibu zote zinazoelekeza Tume ya uchaguzi na kuahidi kutowanyima wananchi haki yao ya kujiandikisha kwa kila mwenye kukidhi vigezo kisheria.