Zenj FM

ZEC, inatarajia kuandikisha Wapiga Kura Wapya 78,922 waliotimiza umri wa miaka 18

17 January 2025, 6:34 pm

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC ,Jaji George J. Kazi akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Wadau wa Uandikishaji wa Wapiga Kura Wapya Awamu ya pili kwa mwaka 2025 katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi uliopo Wete-Pemba.

Na Mary Julius.

Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), inatarajia kuandikisha Wapiga Kura Wapya 78,922 waliotimiza umri wa miaka 18 kwa mujibu wa takwimu ya Sensa na Makaazi ya mwaka 2022 katika Uandikishaji Wapiga Kura Awamu ya Pili kwa mwaka huu wa 2025.
Mwenyekiti wa Tume hiyo,Jaji George J. Kazi ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa Wadau wa Uandikishaji wa Wapiga Kura Wapya Awamu ya pili kwa mwaka 2025 katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi uliopo Wete-Pemba.
Amesema Uandikishaji huo ni matayarisho ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 pia ni Uandikishaji wa mwisho kuelekea katika Uchaguzi huo.
Akizungumzia lengo la kufanya Mkutano huo amesema, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ina utaratibu wa kukutana na wadau kila linapotokea jambo muhimu ambalo linahitaji kushirikisha Wadau hao, sambamba na hilo Tume kupitia Mikutano hiyo inasikiliza maoni, hoja na mapendekezo yatakoyosaidia kuendesha zoezi hilo kwa ufanisi.
Amewaomba wananchi waliotimiza sifa kujitokeza kutumia haki yao ili waweze kushiriki katika Uchaguzi wa mwaka 2025 na kuwakumbusha kwamba huduma za Uendelezaji a Daftari zinaendelea katika Afisi za Tume ya Uchaguzi za Wilaya muda na saa za kazi.
Aidha Amewaomba wananchi na wadau wote wa Uchaguzi wa Zanzibar kudumisha Amani katika kipindi chote cha Uandikishaji wa Wapiga Kura Wapya kama walivyofanikisha katika kisiwa cha Pemba na matumaini yake kwamba wataendelea kushirikiana katika mustakabali mwema wa Uchaguzi wa taifa.

Sauti ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zaznibar,Jaji George J. Kazi

Akiwasilisha taarifa na Utaratibu wa Uandikishaji wa Wapiga Kura Wapya na Uendelezaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Mkurugenzi wa Uchaguzi Thabit Idarous Faina amesema Tume ya Uchaguzi Zanzibar inatarajia kuweka wazi orodha ya wapiga kura waliopoteza sifa na wanaohamisha taarifa zao kama inavyoelekezwa katika kifungu cha 19 na 31 cha Sheria ya Uchaguzi na 4 ya mwaka 2018 wakati wa uwekaji wazi wa Orodha ya wapiga kura walioandikishwa katika uandishaji wa awamu ya pili.

Sauti ya Mkurugenzi wa Uchaguzi Thabit Idarous Faina.

Naye Maulid Ame Mohammed Mkuu wa Kurugenzi ya Huduma za Sheria akiwasilisha mada ya nafasi ya Sheria katika Uandikishwaji na Uendelezaji wa Daftari la wapiga kura amesema kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kila Mzanzibar aliyetimiza miaka 18 ana haki ya kujiandikisha na Kupiga Kura katika Uchaguzi unaofanyika Zanzibar.

Sauti ya Maulid Ame Mohammed Mkuu wa Kurugenzi ya Huduma za Sheria.

Akifunga Mkutano huo wa Wadau Kamishna wa Tume hiyo Awadh Ali Said amewataka wadau kujitambua majukumu yao pamoja na kuwa wakweli katika changamoto zinazojitokeza wakati wa Uandikishaji ili zoezi hilo lifanyike kwa ufanisi bila ya uvunjifu wa amani Visiwani Zanzibar.

Kwa upande wake Juma Kombo Hijja (Sibure) ambae ni Mratibu kutoka Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (UWZ) amevishauri Vyama vya Siasa kuwahamasisha Wapiga Kura kwa kauli za kistaarabu na sio kutoa kauli ambazo zinaviashiria vya uvunjifu wa amani kwani viashiria hivyo vitasababisha kundi la Watu Wenye Ulemavu kutojitokeza katika zoezi la Uandikishaji Wapiga Kura.
Mkutano huo umeshirikisha wadau mbalimbali wa Uchaguzi ikiwemo Taasisi za Serikali na Binafsi, Vyama vya Siasa,Makundi Maalum, Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Vyombo vya Habari.