Kati ya baa 93, baa 33 zimefanikiwa kufunga vizuia sauti Zanzibar
5 December 2024, 5:40 pm
Na Mary Julius.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Masoud Ali Mohammed amesema Zanzibar kuna jumla ya maeneo yanayotoa huduma ya Vileo (baa) 93 ambayo yamesajiliwa na kupewa leseni ya kufanya biashara ya vileo kwa mwaka 2024.
Waziri Masoud ameyasema hayo katika kikao cha Baraza la Wawakilishi Chukwani, Zanzibar, wakati akijibu swali la mwakilishi Jimbo la Mwanakwerekwe Ameir Abdalla Ameir lenye sehemu 3 aaliye taka kujua (a) Zanzibar kuna baa ngapi ambazo zimesajiliwa rasmi.
(b) Je, ni vigezo gani na utaratibu upi hutumika kuzisajili baa hizo.
(c) Je, ni baa ngapi kati ya hizo zimetimiza sharti la vizuizi sauti na ngapi bado hazijatimiza.
Waziri amesema usajili na utoaji wa leseni kwa biashara ya uuzaji wa vileo hutolewa kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti Vileo namba 9 ya mwaka 2020 .
Aidha amesema,maeneo yanayotoa huduma ya Vileo (baa) 33 kati ya maeneo 93 ndiyo yaliyotimiza sharti la kufunga vizuia sauti na maeneo 60 hayajatimiza sharti hili ambapo Serikali tayari imeshayafungia kupiga mziki.