Wazazi waaswa kuwapatia huduma za msingi watoto wenye ulemavu
22 November 2024, 7:25 pm
Na Mary Julius
Mwakilishi viti maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM anayewakilisha kundi la watu wenye ulemavu Mwantatu Mbaraka Khamisi amewataka wazazi kuwapatia huduma za msingi watoto wenye ulemavu kuwajenga kutokana na ulemavu wao ili nao waweze kujitegemea.
Akizungumza huko Forodhani katika tamasha la michezo kwa watoto wenye ulemavu lililoandaliwa na Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar Mwantatu amesema ni faraja kucheza na watoto wenye ulemavu ambao mara nyingi wamekuwa hawashiriki katika mambo ya kijamii.
Aidha amewataka wazazi kutambua kuzaa watoto wenyeulemavu ni majaliwa ya Mungu lakini kuwa na ulemavu sio mwisho wa maisha na kwa kulitambua hilo serikali ya mapinduzi ya Zanzibar imejitoa ilikuona kila mtu anapata huduma za msingi.
Akizungumzia Mradi wa Huduma za Marekebisho kwa Watoto wenye Ulemavu CBR amewaomba wafadhili kusaidia umoja wa watu wenye ulemavu hasa katika program hiyo ili waweze kuwafikia watoto majumbani nakuona watoto wote wanapatiwa huduma na badae wawezekujitegemea.
Mkurugenzi wa Umoja wa Watu Wenyeulemavu Zanzibar Asia Abdulsalam Hussein amesema kuelekea siku ya watu wenye ulemavu duniani disember 3, umoja huo umeanda shughuli mbalimbali ikiwemo ya kuwakusanya watoto wasio na ulemavu kwa kuwajumuisha na watoto wenye ulemavu ili nao wajione kama watoto wengine pamoja na kuwahamasisha wazazi kuwatoa na kuwapatia watoto wenye ulemavu mahitaji yao ya masingi.
Akizungumzia mradi wa Huduma za Marekebisho kwa watoto wenye ulemavu CBR Mkurugenzi Asia amewaomba wafanyabiashara na wafadhili kufadhili mradi huo ili kuweza kuwafikia watoto majumbani na kujua changamoto zao pamoja na kuwasogezea huduma za mazoezi.
Kwa upande wao wazazi wa watoto wenye ulemavu wamewashukuru Umoja wa Watu Wenye ulemavu kwa kuwatoana kujumuika na watoto wenzao ambapo wamepata faraja ya kuona kuwa kuna watu wanawajali.
Aidha wazazi hao wameahidi kuwapatia watoto wao mahitaji muhimu kadri ya uwezo wao pamoja na kuwatoa nje ili wajumuike na watoto wenzao.
Lazziz Bakery ni wafadhili walio dhamini tamasha hilo kwa kutoa chakula kwa watoto wenye ulemavu wamesema wamefadhili tamasha hilo ili watoto hao wajisikie na kujiona wapo sawa na wengine.