Zenj FM

Askari wa KVZ aliyedaiwa kupotea apatikana akiwa amefariki

28 September 2024, 9:47 am

Na Omary Hassan

Askari wa Kikosi cha Valantia (KVZ) SGT Haji Machano Mohamed ambaye inasemekana alipotea akiwa katika Mafunzo ya Uongozi (Afisa Cadet) tangu Agosti 8, 2024 ameonekana jana akiwa amefariki dunia.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Daniel Shillah Tunguu Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, amesema mwili wa marehemu umeonekana Septemba 26,2024 majira ya saa 10.00 jioni katika msitu uliopo karibu na kambi ya chuo cha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Uchumi huko Dunga katika Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Kamanda Shillah amesema kuwa jeshi la polisi kwa kushirikiana na ofisi ya Mkemia Mkuu inaendelea kufanya uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini sababu ya kifo cha askari huyo na hatimaye kuendelea na hatua zingine za kisheria.