Walimu Zanzibar watakiwa kutumia mtaala mpya
14 March 2024, 4:03 pm
Na Ishaka Mohammed Pemba
“Baada ya mafunzo jukumu kubwa la mwalimu ni kutumia mtaala huo wakati wa ufundishaji” Amesema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Leila Mohamed Mussa.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Leila Mohamed Mussa amesema ili mtaala mpya wa elimu ya maandalizi na msingi utekelezeke ni wajibu walimu kubadilika na kwenda sambamba na miongozo ya mtaala huo.
Waziri Leila ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya awamu ya pili ya mtaala na umahiri kwa walimu wa madarasa ya skuli za maandalizi na msingi uliofanyika Mizingani wilaya ya Mkoani Pemba.
Kwa upande wake Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Mohamed Nassor Salim amewataka maofisa wa elimu wa mikoa na wilaya kushiriki muda wote kwenye mafunzo hayo kwani wao ndio wakaguzi wakuu wa elimu katika Wilaya zao.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Elimu Zanzinar Abdalla Mohamed Mussa na Mkaguzi Mkuu wa Elimu Zanzibar Rashid Abdul-aziz Muki wameeleza.
Mafunzo hayo ni maalum kwa ajili ya kuwajenga walimu juu ya mtaala na umahiri juu ya mtaala huo mpya wa elimu ya maandalizi na msingi Zanzibar yatafanyika kwa muda wa siku 5.