Taka kuwa biashara Zanzibar
12 September 2023, 1:28 pm
Timu ya wataalam kutoka Jumuiya ya Mameya wa Afrika ya Kusini (AMALI) wametoa mafunzo namna ya kutenganisha taka ngumu na taka nyepesi.
Na Mary Julius.
Mstahiki Meya wa Jiji la Zanzibar Mahmoud Muhammed Mussa amevitaka vikundi vya usafi kutenga fungu kwa ajili ya kukodi magari yatakayowezesha kufanikisha ukusanyaji wa taka.
Mstahiki meya ameyasema hayo katika mafunzo ya kuwajengea uelewa wenyeviti wa vikundi vya usafi na watendaji wa baraza hilo juu ya kuchakata taka yaliyotolewa na taasisi ya wanaharakati wa mazingira wa Nipe Fagio kutoka Dar es Salama na wataalam kutoka Jumuia ya Mameya wa Afrika ya Kusini (AMALI) katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za baraza la jiji Michenzani wilaya ya Mjini.
Amesema changamoto kubwa wanayokumbana nayo katika kuliweka jiji la Zanzibar safi ni usafirishaji wa taka kutoka maeneo mbalimbali hivyo kukodishwa kwa gari hizo kutasaidia usafirishaji wa taka kutoka majumbani na kuzipeleka maeneo yanayostahili lengo likiwa ni kuliweka jiji la Zanzibar safi na salama.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Jiji Zanzibar kupitia huduma za jamii, Abdullatif Omar Haji amesema kutokana na changamoto ya ulipaji wa taka kwa baadhi ya wananchi wataishauri serikali kuandaa utaratibu wa kulipisha ada ya taka kwa kupitia bili za Zeco.
Nao wadau kutoka Dar es Salaam wa taasisi ya Nipe Fagio wamesema lengo la kuja Zanzibar ni kuhakikisha wanatoa elimu ya uchakataji wa taka pamoja na kuandaa sehemu itakayotumika kupokea taka kutoka sehemu mbalimbali za jiji la Zanzibar ili kufikia taka sifuri .