Swebe: CCM acheni uoga CHADEMA tunawanyima usingizi
28 May 2024, 15:58
Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Kyela Victoria Swebe amekitaka Chama Cha Mapinduzi CCM kuacha uoga wa kiasiasa badala yake wajitokeze hadharani katika kuwahudumia wananchi.
Na Masoud Maulid
Saa chache baada ya Chama Cha Mapinduzi CCM Kyela kutangaza kuwapokea wanachama wapya kutoka CHADEMA, Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimekanusha taarifa za wanachama wake kata ya Kajunjumele kujiunga na CCM.
Katika taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Kyela Victoria Swebe amesema taarifa zinazoenezwa na viongozi wa CCM kuwapokea wanachama kumi na watano kutoka Chadema si za kweli na kuwa watu hao ni wanachama wa vyama vingine vya siasa na si CHADEMA.
Swebe ameongeza kuwa hakuna mwanachama wa Chadema ambaye amehamia CCM kwa kuwa wanachama wa CHADEMA wapo imara na hata anayetajwa kujiunga na CCM amewahi kuwa kwenye vyama vingine vya upinzani ikiwemo NCCR-Mageuzi hivyo Chadema haijapoteza wanachama kwa idadi ambayo imetajwa na viongozi wa CCM.
Katika hatua nyingine mwenyekiti huyo ameongeza kuwa,chama cha mapinduzi ni chama kikongwe hapa nchini Tanzania,hivyo viongozi wake waache uoga badala yake wafanye kazi za wananchi na si kujinadi juu ya kuvuna wanachama wa chadema ambapo matokeo yake ni kuipaisha chadema na kuonesha inawanyima usingizi muda wote.
Kuelekeza uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu hapa nchini Tanzania imekuwa ni kawaida kwa baadhi ya wanachama kutoka vyama mbalimbali kuhama vyama vyao na kujiunga na vyama vingine.