Kyela:Mwanjala atembelea Convenant Edible Oil
23 March 2024, 22:28
Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi kyela akiambatana na kamati yake ya siasa wilaya ya Kyela amekagua kiwanda kipya cha kuzarisha mafuta cha Convenant Edible Oil na kumwagia sifa lukuki mwekezaji wa kiwanda hicho.
Na Nsangatii Mwakipesile
Kamati ya siasa ya chama cha mapinduzi wilaya ya Kyela ikiongozwa na Mwenyekiti wake Elias Mwanjala imefanya ziara yake leo ya kichama na kukagua miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho.
Katika msafara huo Mwanjala ameongozana na mkuu wa wilaya ya Kyela Josephine Manase,Mwenyekiti wa halmashauri Katule Kingamkono,mkurugenzi mtendaji wa halmashauri pamoja na wakuu wa idara mbalimbali hapa wilayani kyela.
Akizungumza akiwa katika kiwanda cha kuzarisha mafuta Convenant Edible Oil kinachotengeneza mafuta ya kula ya Kyela Coking Oil Mwanjala amempongeza mkurugenzi wa kiwanda hicho Babylon Mwakyambile kwa kuamua kuanzisha kiwanda hicho kwani imefungua milango ya ajira kwa vijana jambo ambalo litapunguza ukwasi wa ajira hapa nchini na hapa wilayani.
Kwa upande wa mkuu wa wilaya ya Kyela Josephine Manase amesema uwekezaji huo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la serikali lililotolewa na Raisi wa jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa viongozi kuhakikisha wanasimamia upatikanaji wa mafuta ya kula ili kuondokana na kadhia ya uagizwaji wa mafuta nje ya nchi.
Naye mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kyela Katule Kingamkono mbali na kupongeza lakini pia ameshauri mwekezaji wa kiwanda hicho Babylon mwakyambile kuwepo vifaa vinavyoendana na mazingira ya kiwanda ili kuondoa madhira yanayoweza kujitokeza wakati shughuli za uzarishaji zikiendelea.
Akisoma taarifa ya kiwanda hicho msemaji wa kiwanda cha Convenant Edible Oil kinachotengeneza mafuta ya kula ya Kyela Coking Oil Emmanuel Jotham amesema kiwanda hicho kimesajiliwa na shirika la viwanda vidogovidogo SIDO ambapo uwekezaji wake unagharimu shilingi bilioni moja na milioni miatatu ambapo kuwepo kwa kiwanda hicho kunatarajiwa kupunguza adha ya ajira kwa watanzania
Ziara hiyo imehitishwa baada ya kukagua na kutembelea jumla ya miradi nane ambayo ni skimu ya umwagiliaji Makwale,kukagua wodi ya mama na mtoto kata ya Ngusa,shule ya wasichana Busale,shule ya sekandari Ibanda,bwawa la samaki,kukagua jengo la mama na mtoto hospitali ya wilaya ya Kyela pamoja kiwanda cha Convenant Edible Oil kinachotengeneza mafuta ya kula ya Kyela Coking Oil.