Kyela:Wenye 3d Kyela sasa kukiona cha moto
20 March 2024, 11:44
Mkuu wa usalama barabarani wilayani kyela Assistant Inspecta Seif amewataka madereva ambao bado hawajatoa pleti namba za 3d kutoingiza magari yao barabarani mpaka hapo watakapotekeleza agizo hilo.
Na James Mwakyembe
Jeshi la polisi wilayani kyela kitengo cha usalama barabarani limesema litawasaka popote wamiliki binafsi na biashara wa vyombo vya moto ambao bado hawajatoa pleti namba za 3d.
Kauli hiyo inakuja kufuatia marufuku iliyotolewa na jeshi la polisi hapa nchini likiwataka wamiliki binfsi na biashara wa vyombo vya moto kuondoa kwa ridhaa yao pleti namba za 3d katika kipindi cha majuma mawili ambayo tayari yamekwisha tamatika.
Akizungumza akiwa ofisini kwake Assistant Inspecta Seif mkuu wa usalama barabarani wilaya ya Kyela amesema kwa muujibu wa taarifa jeshi la polisi hapa nchini muda wa wiki mbili zilizotolewa tayari umekwisha hivyo kuwataka wamiliki na madereva ambao bado hawajatoa pleti namba hizo kutoingiza magari yao barabarani la sivyo sheria itafuata.
Akitoa taarifa ya usalama barabarani Assistant Inspecta Seif mkuu huyo wa usalama barabarani wilaya ya Kyela amesema katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita kumekuwa na ajari ndogondogo zinazosababishwa na umakini mdogo wa waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda.
Katika hatua nyingine Assistant Inspecta Seif amewataka madereva wote hususani waendesha pikipiki maarufu bodaboda kufuata na kutii sheria za usalama barabarani kwani kama jeshi la polisi halifurahishwi na uwepo wa baadhi ya madereva wanaokiuka sheria wawapo barabarani.
Amehitimisha kwa kusema bado wanaendelea na oparesheni ya kukamata vyombo vya moto ambavyo madereva wake hawataki kufuata sheria na kusisitiza kuwa jeshi hilo halitamvumilia dereva yeyote mwenye kuvunja sheria awapo barabarani.