Muzdalifa yaiomba serikali kuanzisha siku ya mtoto yatima
10 December 2024, 6:54 pm
Na Berema Nassor.
Taasisi ya Muzdalifa Charitable Organization Zanzibar wameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuweka mpango madhubuti ya kuiweka siku ya maadhimisho ya mtoto yatima Zanzibar katika kalenda ya matukio ya kitaifa kwa lengo la kuwatambua na kuwafariji watoto mayatima kitaifa hapa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Katibu Mkuu wa Taasisi hiyo Farouk Hamad Khamis katika ofisi za taasisi hiyo iliyopo amani kuelekea maadhimisho ya saba ya mtoto yatima Zanzibar amesema licha ya jitihada mbali mbali zinazochukuliwa na taasisi binafsi katika kuhamasisha jamii juu ya kuwalea na kuwahurumia watoto hao lakini bado wanakumbana na changamoto kadhaa za vitendo vya udhalilishaji ikiwemo kukosa haki zao za msingi kutoka kwa wazazi wao waliofariki.
Amesema taasisi hiyo ipo mstari wa mbele katika kuchukua juhudi na bidii za kuelimisha jamii juu ya kuwalea watoto mayatima katika malezi yaliyo bora.
.Kwa upande wake Mratibu wa Asasi za Kiraia Mahfoudh Shaaban Haji ambae pia ni mratibu wa maadhimisho hayo amesema lengo kubwa la kufanya madhimisho hayo ni kutaka kuwekwa katika kalenda ya kitaifa sambamba na kuweza kuwathamini na kuwafariji watoto mayatima hivyo kupitia tasisi hiyo imeona kwamba ni vyema kutenga siku maalum kwa ajili ikiwa ni miongoni mwa kuadhimisha siku hiyo.
Kilele cha Maadhimisho ya saba ya mtoto yatima Zanzibar yanatarajiwa kufanyika tarehe 14 mwezi huu chini ya tasisi ya Muzdalifa charitable Organization Zanzibar ikishirikiana na wadau mbalimbali ambapo kauli mbiu ya maadimidhimisho hayo ni KILA MTOTO ANASTAHIKI KUWA NA FAMILIA BORA.