Mwanamke Initiatives, Oryx yatua mizigo ya kuni kaya 785 Panza Pemba
13 November 2024, 6:27 pm
Na Is-haka Mohammed.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud amewataka wananchi wa Kisiwapanza kutumia vyema mitungi ya gesi waliyokabidhiwa kwani imelenga kuwaondoshea changamoto za athari za kimazingira zinazoendelea kukikumba kisiwa hicho
Mattar ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kisiwapanza kilichopo Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba katika hafla ya kukabhidhi jumla ya mitungi 785 ya gesi kwa kaya zote zilizopo katika kisiwa hicho.
Amesema lengo kubwa la kupewa mitungi hiyo ni kuweza kuitumia pamoja na kuachana na ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa kwani zimekuwa zikisababisha athari kubwa za kimazingira na kiafya kwa wakaazi wa Kisiwapanza.
Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation Sabra Ali Mohamed amesema wanawake wa visiwa vidogo vidogo hapa Zanzibar wamekuwa wahanga wakubwa wa matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia pamoja na kukata miti ya mikoko.
Kwa upande wake Meneja wa Kampuni ya Oryx Shuwekha Omar Khamis ameeleza athari zitokanazo na athari za utumiaji wa nishati isiyo safi kwa jamii wakiwemo wananchi wa kisiwa hicho kidogo cha Kisiwapanza.
Wakizungumza mara baada ya kukabidhiwa mitungi hiyo baadhi ya wananchi wa Kisiwapanza wameishukuru serikali na wadau walioshirikiana nao kuwapatia mitungi hiyo na kuahidi kubadilika kwa kuwanza kutumia nishati safi na salama kwao.