Zenj FM

Majengo ya Mjerumani yazusha mzozo Zanzibar

3 November 2024, 3:18 pm

Jengo  lililojengwa na iliokuwa serikali ya Ujerumani Mashariki Zanzibar.

Na Mwandishi wetu

Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC) limetangaza kuwaondoa na kuwahamisha  wakaazi wanaoshi kwenye majengo yaliojengwa na iliokuwa serikali ya ujerumani mashariki Zanzibar  kwa miaka  sitini sasa kwa madai ya kutaka kuvunjwa ili kupisha uwekezaji  mpya. .

Mgogoro  umezuka na kuwaibua watu kadhaa akiwemo  mtoto wa pili  wa  Rais wa kwanza Zanzibar Balozi Ali  Abeid Karume pamoja na mbunge  wa zamani jimbo la Kikwajuni Parmukh Hogan Sigh.

Balozi Karume amesema uamuzi wowote wa kuvunja majengo hayo na wananchi kuhamishwa kwa nguvu, kunaweza kuleta mtafaruku kati ya SMZ na wananchi. 

Balozi Karume amedai yupo mtu ambaye kwa dhamira mbaya  anafikiri  anataka  kuleta ukorofi  ili kuvuruga nia njema ya serikali ya CCM  huku akichochea uvunjifu wa umoja na amani .

Amesema ni vema Shirika la Nyumba  Zanzibar likaelewa sababu za ujenzi wa nyumba hizo,kwanini zilijengwa ,nani mjenzi wake  na zimeachwa chini ya dhamana ipi  baada ya kumalizika kuliko  kufanya watakavyo.

Sauti ya Balozi Ali  Abeid Karume.

Naye Mbunge wa zamani wa kikwajuni Parmukh Singh Hogan amesema  kuvunjwa nyumba hizo ni mwanzo wa kufutwa kwa  historia kati ya ujerumani na Zanzibar pia kwa Jamhuri ya Muungano  sababu wao ndiyo waliojenga baada ya Mapinduzi.

Ujerumani Mashariki ndio taifa la kwanza duniani  kuyatambua Mapinduzi ya Zanzibar  mwaka 1964 ikafuatia China,baadae Cuba yakafuata mataifa  mengine  mengine duniani .

Sigh  amesema ni busara endapo ujerumani itashirikishwa kwani hata aliookuja kiongozi wake kutembelea Zanzibar, alifika kuona majengo  hayo hivyo haitakuwa sahihi kudhoofisha mahusiano ya taifa na taifa .

Sauti ya Mbunge wa zamani wa kikwajuni Parmukh Singh Hogan.

Kwa upande  mwingine  Mwenyekiti wa kamati ya kufuatilia mgogoro huo Jaha Ame Rajab ,amesema tayari  wananchi wakaazi  wa eneo hilo wameshaanza vikao vya kujadili suala hilo na viongozi wa SMZ .

Jaha amesema mkuu wa wilaya ya mjini Rashid Masaraka ameshakutana na kamati  yake hivyo kuna mfululizo wa  vikao vinavyoendelea lakini akasema bado haijajulikana hatma ya jambo hilo .

Amesema mahali hapo wanaishi watu   toka  awamu ya utawala wa  kwanza wa SMZ  hivyo uamuzi wowote wa kuwafukuza, unaweza kuamsha chuki,hamaki na mzozo mkubwa usiokwisha.

Sauti ya Mwenyekiti wa kamati ya kufuatilia mgogoro huo Jaha Ame Rajab

Nacho Chama cha ACT wazalendo kimesema uwamuzi wa huo  ni kinyume na haki  za binadamu lakini pia unapuuzia  malengo ya Rais wa kwanza Abedi Amani Karume ya kuwapatia makaazi bora wananchi.

Waziri kivuli wa ardhi ACT Wazalendo…Rashid Ali Abdalla..amesema ingekuwa busara sana iwapo wananchi watashirikishwa na kutoa maoni yao kabla ya kupitishwa maamuzi mengine. 

Sauti ya Waziri kivuli wa ardhi ACT Wazalendo…Rashid Ali Abdalla.

Nyumba za maghorofa Kikwajuni zilijegwa baada ya mapinduzi kama msaada wa kuwapatia makaazi bora wananchi na serikali ya ujerumani Mashariki.