Zenj FM

Usawa wa kijinsia suala lenye maswali lukuki kwenye nafasi za uongozi

25 October 2024, 7:36 pm

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Rahma Kassim Ali katika picha ya pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Riziki Pembe Juma huko Baraza la Wakilishi Chukwani Zanzibar.

Na- Ivan Mapunda.

Hadi sasa ni nchi 22 tu zina mwanamke kama mkuu wa nchi au serikali na katika nchi 119 hawajawahi kupata fursa hiyo jambo ambalo lina athari kubwa kwa matakwa ya wasichana wanaokua.

Tanzania ni miongoni mwa nchi hizo 22 ambazo zina viongozi wakuu katika nchi na serikali  akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Spika wa Bunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Tulia Akson.

Takwimu zinaonyesha kwamba mwaka 1995, wakati mfumo wa vyama vingi ulipoanza idadi ya wanawake waliokuwa wakijitokeza kuwania uongozi kwenye uchaguzi mkuu ilikuwa ndogo.

Sasa hivi siyo kama zamani,walau wanawake wanafurukuta na wameweza kushika nafasi mbalimbali za uongozi, zikiwemo za juu katika nchi na serikali.

Kwa mara ya kwanza tangu mapinduzi matukufu ya Zanzibar, huku ikiwa inasheherekea miaka 61 ikiwa na Katibu Mkuu kiongozi wa Baraza la Mapinduzi Mhandisi  Zena Saidi.

Wanawake wengine waliowahi kushika nafasi za juu na wanaoshika nafasi hizo ni  Naibu Spika wa  Baraza la wawakili , Mgeni Hassan , pia wapo baadhi ya mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na makatibu wakuu na masheha.

Takwimu zinaonyesha kwamba mwaka 1995, wakati mfumo wa vyama vingi ulipoanza idadi ya wanawake waliokuwa wakijitokeza kuwania uongozi kwenye uchaguzi mkuu ilikuwa ndogo.

Ila sasa hivi katika baraza la wawakilishi ni wanawake nane tu waliojitosa majimboni ambao walishinda uwakilishi , wanawake 18 walipata uwakilishi kupitia nafasi za viti maalum na hivyo kufanya idadi ya wanawake baraza la wawakilishi  kuwa 29 kati ya 77 waliochaguliwa, sawa na asilimia 40.

Dorothy Temu Usiri ni Mratibu wa Umoja wa Mataifa -UN hapa Zanzibar amesema malengo ya millennia hayajaweza kufikiwa.”licha ya kuwa tumejihidi kupiga hatua, bado hatukuweza kufikia usawa wa kijinsia wa 50 kwa 50 wanawake kwa wanaume kwenye uongozi,” Amemaliza Dorothy.

Kukwama huko kumewalazimisha wanawake duniani kutengeneza malengo mengine mapya yenye kauli mbiu ’50 kwa 50 ifikapo 2030, tuongeze jitihada.

Wanaharakati wa masuala ya kijinsia nchini wanasema vipo vikwazo vingi vinavyokwamisha jitihada za wanawake kiuongozi.

Khamis Mbeto Khamis ni Katibu wa kamati maalum ya -NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na mafunzo kutoka Chama cha mapinduzi -CCM Zanzibar amesema CCM inatoa fursa sawa katika kugombea nafasi mbalimbali kama katiba ya chama hicho inavyoeleza kuwa kila mwanachama ana haki ya kugombea nafasi yoyote ile kuanzia ngazi tawi mpaka taifa lakini ikaona haitoshi ikaweka nafasi ya upendeleo kwa wanawake ya kuweka viti maalum kwa ajili yao.

Katika muktadha huo anasema: “Hali hii inawezekana na ni lazima ibadilike, kinachohitajika ni utashi wa kisiasa kusaidia kikamilifu na kwa makusudi uwakilishi wa wanawake na wanawake wenyewe kuchangamkia fursa hiyo ya kugombea nafasi mbalimbali kama katiba inavoeleza na kuacha kusubiri nafasi za viti maalum.” Amemaliza Mbetto.

Khamis Mbetto ameongeza kuwa kuwa bado zinahitajika nguvu za ziada ili kuweza kuyafikia malengo yaliyopangwa na hilo litawezekana kama wanawake wenyewe wataungana mikono kama sasa hivi umoja wa wanawake wa Umoja wa Wanawake Tanzania -UWT walivyokuwa na kauli mbiu yao ya rafiki wa mwanamke ni mwanamke mwenzie.

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA- Zanzibar Dkt Mzuri Issa amesema dhana potofu kuhusu adui wa mwanamke ni mwanamke mwenzake katika  harakati za kumkomboa mwanamke, pia zinachangia kurudisha nyuma malengo ya millennia.  “Utashangaa kipindi cha uchaguzi mwanamke anakuwa adui namba moja wa mwanamke mwenzake, hili ni tatizo ambalo litatufanya tuendelee kusota,”Amesema Dkt Mzuri.

Dkt Mzuri ameongeza amesema wakati umefika sasa wa kushikana mikono wanawake kwa wanawake kwa sababu rafiki wa mwanamke ni Mwanamke “Tunahitaji  kubadilika na kutafuta marafiki wakiume ambao wanaweza  kuwasapoti wanawake,pamoja  kuyasoma mazingira  , kujiweka katika jamii na kutumia vizuri mitandao pamoja na kujua sera na sheria ili kufika malengo ” Amemaliza Dkt Mzuri.

Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki ambaye anawakilisha Tanzania Nadra Juma Mohamed amesema bado kuna safari ndefu ya kuhakikisha wanawake wanaheshimiwa wanapowania uongozi.

”Licha ya kupambana usiku na mchana bado misukosuko ikiwamo kutukanwa,kudhalilishwa na kudhihakiwa imekuwa kikwazo kwa mwanamke kupata uongozi”Amesema Nadra

Huku akiongezea kuwa ile dhana ya adui wa mwanmke ni mwanamke mwenzie sio kweli kwa sababu katika harakati za kugombania nafasi hiyo ya ubunge asilimia 70 waliomchagua ni wanawake wenzake.

 Mikakati ya kufanikiwa.

 Mkurugenzi Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar ZAFELA, Jamila Mahamoud Juma amesema Jumuiya ya wanasheria wanawake,wanapambana kutengeneza mikakati itakayowasaidia wanawake kutambua nafasi na uwezo wao kwenye jamii, ikiwamo kisiasa.”Tunaendelea kutoa elimu kwa njia mbalimbali katika kuhakikisha wanawake wanatambua uwezo wao,fursa na namna wanavyoweza kubadili sura ya mfumo kandamizi,” Amesema Jamila wakati akizungumza na Mwandishi wa makala hii.

Mgawanyo wa rasilimali kwa usawa na kutoa elimu  kwa wanawake na kuwajengea uwezo wa kujiamini nahii ni miongoni mwa agenda zao katika kufikia mafanikio.

Kwa mfano Azimio na mpango kazi wa Beijing, mkataba wa kimataifa wa kutokomeza aina zote za ukandamizaji na dhuluma dhidi ya wanawake, mkataba wa usawa wa jinsia wa SADC, pamoja na ule wa MAPUTO, hii yote inatulazimisha kujali usawa kijinsia.

Kwa Zanzibar kati ya mawaziri na manaibu mawaziri 30, wanawake ni 9 pekee sawa na 25.7% huku wanaume wakiwa 26 sawa na 74.28%.

Kwa  Tanzania ni nchi ambayo imeridhia mikataba na matamko mengi ya kimataifa yanayosisitiza usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake hususan ushiriki wao katika ngazi zote za maamuzi kimataifa, kikanda na hata sera na miongozo ya kitaifa.