Wakulima wa karafuu watakiwa kuzingatia sheria Pemba
16 July 2024, 7:47 pm
Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar kwa kushirikiana na kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya wataendelea kuwafuatilia wale wanaopita kwa wananchi na kuwahadaa ili wawauzie karafuu na wale ambao watakamatwa watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Wakulima wa karafuu wameombwa kutouza karafuu zao kwa watu wanaopita mitaani kwani jambo hilo licha ya kuwa ni kwenda kinyume na sheria ya maendeleo ya karafuu Zanzibar pia inapelekea kudhulimiwa kwani vipimo vinavyotumika haviendani na pishi za kawaida.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa kiwanda cha mafuta ya makonyo Wawi Chake Chake, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar Sudi Said Ali amesema vipimo vinavyotumiwa na walanguzi hao vina ujazo mkubwa ukilinganisha na pishi ya kawaida.
Akitolea mfano pishi walizozikamata kwa walanguzi wanaopita kununua karafuu kwa wananchi Mkurugenzi amesema moja ni sawa na kilo 2, na nyengine kilo mbili kasorobo huku kipimo cha pishi halali ya karafuu ni kilo moja na robo.
Pamoja na kuwataka wakulima hao kutouza karafuu zao kwa mtu yeyote kwani shirika halijamtuma mtu kwa ajili ya kuwanunulia karafuu na kueleza kuwa wakati huu wakisubiri kuzinguliwa kwa msimu mpya wa karafuu kwa wale walioanza kuchuma karafuu zao wazipeleke kwenye vituo vyao vikuu ambavyo ni Mkoani, Madungu kwa Chake Chake na Wete.
Aidha Sudi amesema wakiwa katika harakati zao za kukagua zao la karafuu katika msimu huu wamebaini kuwapo kwa watu wasiopendelea maendeleo ya mkulimu wamekuwa wakipita mitaani na kununua karafuu zao kinyume na sheria na kwa kutumia vipimo visivyo sahihi.