Zenj FM
Zenj FM
13 April 2026, 4:33 pm

Jumla ya matukio 29 yameripotiwa katika mikoa minne ya Zanzibar yakihusishwa na madai ya watu kushikwa mabega na kupoteza sehemu zao za siri. Kamishna wa Polisi Zanzibar, Kombo Khamis Kombo, amesema uchunguzi umebaini kuwa madai hayo si ya kweli, kwani wote waliodai kuathirika walifanyiwa vipimo na kuthibitishwa kuwa salama.
Na Mary Julius.
Jumla ya matukio 29 yameripotiwa katika mikoa minne ya Zanzibar yakihusishwa na madai ya watu kushikwa mabega na kudai kupoteza sehemu zao za siri, hali iliyozua taharuki kubwa katika jamii.
Akizungumza na vyombo vya habari katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Ziwani, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Kombo Khamis Kombo, amesema Mkoa wa Mjini Magharibi umeongoza kwa matukio 22, huku Kusini Unguja kukiwa na tukio moja, Kusini Pemba matatu na Kaskazini Pemba matatu.
Ameeleza kuwa katika matukio ya Kaskazini Pemba, tukio moja lilisababisha kifo cha Hamad Othman Mwalimu (35), mkazi wa kijiji cha Jojo, ambapo watuhumiwa tayari wanashikiliwa na Jeshi la Polisi.
Hata hivyo, Kamishna Kombo amesisitiza kuwa madai ya kupotea kwa sehemu za siri hayana ukweli wowote.
Amesema wote waliodaiwa kuathirika walipelekwa hospitali na kufanyiwa uchunguzi, na kuthibitika kuwa sehemu zao za siri zipo salama bila athari yoyote.
Amebainisha kuwa uvumi huo unahusishwa na imani za kishirikina na umechangia kusababisha madhara ikiwemo majeraha na hata kupoteza maisha.
Jeshi la Polisi limewataka wananchi kupuuza taarifa hizo zisizothibitishwa na kuacha kuzisambaza, likisisitiza kuwa yeyote atakayebainika kueneza uvumi kwa makusudi atachukuliwa hatua za kisheria.
Aidha, wananchi wametakiwa kutoa taarifa sahihi kwa vyombo vya usalama, kuepuka kuchukua sheria mkononi, na kutumia vyanzo rasmi kupata habari za kuaminika ili kulinda amani na utulivu wa jamii.