Zenj FM
Zenj FM
10/04/2026, 15:07

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi limekanusha vikali taarifa zinazosambaa mitandaoni zikidai kuwepo kwa matukio ya watu kupoteza au kuibiwa sehemu zao nyeti , likizitaja kuwa ni uzushi usio na ukweli. Polisi wamesema watu 10 wanashikiliwa kwa kusambaza taarifa hizo za uongo zilizozua taharuki kwa wananchi.
Na Mary Julius.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi limepinga vikali taarifa za uongo zinazosambaa zikidai kuwepo kwa matukio ya watu kupoteza au kuibiwa sehemu zao za siri, likizitaja kuwa ni uzushi unaozusha hofu na taharuki kwa jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharib Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Richard Mchomvu, amesema watu 10 wanashikiliwa kwa kusambaza taarifa hizo zisizo na ukweli.
Amesema uchunguzi wa kitabibu uliofanyika kwa watuhumiwa wote umebaini kuwa hakuna hata mmoja aliyekuwa na tatizo lolote, hivyo kuthibitisha kuwa madai hayo ni ya kupotosha.
Polisi imeonya wananchi kuacha kusambaza taarifa zisizo na uhakika na badala yake kufuata sheria, ikisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wanaoendeleza uzushi huo.