Zenj FM

Dkt. Khalid atoa wito,waasisi wa taifa waenziwe na kuombewa dua

01/04/2026, 18:27

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Khalid Salum Mohamed akizungumza katika ziara na dua maalum ya kumuombea aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Brigedia Jenerali Mstaafu Ramadhani Haji Faki,

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Khalid Salum Mohamed, amewataka Watanzania kuwaenzi na kuwaombea dua waasisi wa taifa kutokana na mchango wao mkubwa katika kupigania uhuru. Amesema ni muhimu kwa kizazi cha sasa kuendeleza mema waliyoacha kwa kudumisha amani na mshikamano.

Na Mary Julius.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Khalid Salum Mohamed, amesema Watanzania wana wajibu wa kuwaenzi na kuwaombea dua waasisi wa taifa, kufuatia mchango wao mkubwa katika kupigania uhuru na kuleta ukombozi.

Akizungumza katika ziara na dua maalum ya kumuombea aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Brigedia Jenerali Mstaafu Ramadhani Haji Faki, iliyofanyika Mkwajuni, Wilaya ya Kaskazini A, Dkt. Khalid amesema waasisi hao walifanya kazi kubwa na ngumu ya kupigania haki za wengi na kuleta usawa katika jamii.

Ameeleza kuwa ni jukumu la kizazi cha sasa kuyaenzi na kuyaendeleza mema yote yaliyoachwa na viongozi hao, huku akiwahimiza vijana kukumbuka historia yao na walipotoka, pamoja na kuimarisha amani, upendo na mshikamano nchini.

Sauti ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Khalid Salum Mohamed.

Kwa upande wake, mtoto wa pili wa marehemu, Ali Ramadhani Haji, amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa juhudi zake za kuenzi fikra za waasisi wa mapinduzi kwa vitendo.

Aidha, amemshukuru kwa kujenga skuli ya kisasa katika mkoa wa kaskazini iliyopewa jina la marehemu.

Sauti ya Ali Ramadhani Haji.