Zenj FM
Zenj FM
23/03/2026, 16:31

Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Mudrik Ramadhani Soraga, amesema serikali imefanikiwa kutoa mafunzo ya TEHAMA kwa wananchi zaidi ya 7,500 kupitia vituo vya TEHAMA jamii Unguja na Pemba.
Na Mary Julius.
Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Mudrik Ramadhani Soraga, amesema Wizara imefanikiwa kutoa mafunzo ya TEHAMA na ujuzi wa kidijitali kwa wananchi 282 kupitia vituo vya TEHAMA Jamii vilivyojengwa katika kila wilaya za Unguja na Pemba.
Waziri Soraga ameeleza kuwa lengo la programu hiyo ni kuhakikisha kila mwananchi anashiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali (Inclusive Digital Economy), ili kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia matumizi ya teknolojia.
Ameyasema hayo alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa kipindi cha siku 100 katika Ukumbi wa Habari Maelezo, Raha Leo.
Aidha, Waziri huyo amebainisha kuwa tangu kuanzishwa kwa vituo hivyo, zaidi ya wananchi 7,500 tayari wameshapatiwa mafunzo mbalimbali ya TEHAMA, hatua inayodhihirisha mafanikio ya Serikali katika kupanua wigo wa matumizi ya teknolojia kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, amesema Serikali imeanzisha mfumo wa kidijitali unaojulikana kama Zanzibar Government Services Directory (ZGSD) unaowezesha Wizara na taasisi mbalimbali kusimamia na kuweka taarifa za huduma za Serikali kwa njia ya kidijitali. Jumla ya huduma 42 zinatarajiwa kutolewa kupitia mfumo huo, ambapo hadi sasa Wizara na taasisi 17 tayari zimeshawasilisha taarifa zao.
Pia, Wizara imekamilisha maandalizi ya Sera ya Kidijitali ya Zanzibar ya mwaka 2026, huku e-Government Authority Zanzibar (eGAZ) ikiwa katika hatua za mwisho za kuandaa miongozo ya matumizi salama na yenye uwajibikaji ya Teknolojia ya Akili Unde (AI).
Kuhusu miundombinu ya TEHAMA, Waziri Soraga amesema Serikali inaendelea na jitihada za kuanzisha mradi wa mji wa kisasa wa kidijitali (Smart City) katika eneo la Fumba, ambapo inaendelea kutafuta wawekezaji kupitia taasisi husika.
Aidha, huduma za mawasiliano zinaendelea kuboreshwa katika visiwa vidogo kupitia ujenzi na uimarishaji wa minara ya mawasiliano katika maeneo ya Tumbatu, Kojani, Fundo na Kokota. Sambamba na hilo, mradi wa ujenzi wa minara 35 unaendelea kutekelezwa katika Unguja na Pemba ili kuboresha upatikanaji wa huduma za mawasiliano.
Katika kuimarisha mifumo ya utawala bora wa kidijitali, Waziri Soraga amesema jumla ya anuani 533,386 zimeshatolewa na kusajiliwa kidijitali, huku vishkwambi 388 vikisambazwa katika Unguja na Pemba, kimoja kwa kila shehia, ili kurahisisha utoaji wa huduma na shughuli za kijamii na kiuchumi.