Zenj FM

Polisi Kusini Unguja watoa tahadhari kabla ya sikukuu ya Eid

19/03/2026, 20:24

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Daniel Emmanuel Shillah.

Kamanda wa Polisi Kusini Unguja, SACP Daniel Shillah, amewahimiza wananchi kusherehekea Eid kwa utulivu huku Jeshi la Polisi likiahidi kuimarisha ulinzi na usalama.

Na Mary Julius.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Daniel Emmanuel Shillah, amewataka wananchi kusherehekea sikukuu ya Eid El-fitr kwa amani na utulivu, huku akisisitiza umuhimu wa kudumisha mshikamano na kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha usalama na uvunjifu wa amani.

Ametoa wito huo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Kamanda huko Kusini Unguja, SACP Shillah amesema Jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarishwa katika kipindi chote cha sikukuu hiyo.

Aidha, amewasihi wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa pindi wanapoona viashiria vya uhalifu au vitendo visivyo vya kawaida, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa haraka.

Amesema, Jeshi la Polisi linaendelea kutoa wito kwa watumiaji wa barabara kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika wakati wa msimu huu wa sikukuu.

Sauti ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Daniel Emmanuel Shillah.