Zenj FM

Polisi wafichua mbinu mpya za matapeli kabla ya Eid

19/03/2026, 19:55

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharib, Richard Thadei Mchomvu, akionyesha mfano wa kitambulisho ambacho hutumia na matapeli katika kuwaanganya watu.

Na Mary Julius.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi limewakamata vijana watano wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu wa kimtandao, wakiwemo matapeli wanaojifanya mawakala wa huduma za simu au kutoa ajira ili kuwaibia wananchi fedha kwa njia ya udanganyifu.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Polisi Madema, Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Richard Thadei Mchomvu, amesema kuwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao ni sehemu ya operesheni maalum inayoendelea kupambana na uhalifu huo unaozidi kuathiri jamii.

Ameeleza kuwa pamoja na mbinu hizo, wahalifu wamekuwa wakitumia simu zilizoibwa kuwatapeli ndugu na marafiki wa wahanga, hali inayosababisha hasara kubwa kwa wananchi.

Kutokana na hali hiyo, Kamanda Mchomvu amewataka wananchi kuwa makini kwa kutokutoa taarifa zao binafsi kwa watu wasiowafahamu, pamoja na kutoa taarifa mara moja kwa vyombo vya dola wanapobaini vitendo vya uhalifu.

Sauti ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharib, Richard Thadei Mchomvu,.

Akizungumzia maandalizi ya kuelekea sikukuu ya Eid El Fitri, amesema Jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu kuimarisha ulinzi katika maeneo yote muhimu, ikiwemo maeneo ya ibada, viwanja vya mikusanyiko ya watu pamoja na maeneo ya kijamii, ili kuhakikisha sikukuu hiyo inaadhimishwa kwa amani na utulivu.

Amefafanua kuwa katika kipindi chote cha sikukuu, kutakuwepo na doria na misako ya mara kwa mara itakayohusisha askari wa miguu, magari, pikipiki pamoja na vikosi maalum ikiwemo kikosi cha mbwa na farasi kwa lengo la kudhibiti vitendo vya uvunjifu wa amani.

Aidha, wananchi wameaswa kuchukua tahadhari wanaposherehekea sikukuu hiyo kwa kulinda mali zao, kuepuka kuondoka majumbani kwa pamoja, pamoja na kufuatilia mienendo ya watoto wao ili kuepusha vitendo vya kihalifu.

Katika kuhakikisha usalama barabarani unaimarika, Jeshi la Polisi limetangaza kufungwa kwa muda kwa baadhi ya barabara, hususan zile zinazoelekea Kariakoo na maeneo ya katikati ya mji, ili kurahisisha shughuli za sikukuu.

Sauti ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharib, Richard Thadei Mchomvu.