Zenj FM
Zenj FM
06/03/2026, 16:46

Na Hakika Mwinyi.
Kamati za kukabiliana na maafa zimetakiwa kuwa na uelewa mpana kuhusu hatari zinazoweza kujitokeza katika jamii, hususan katika kipindi hiki cha mvua za masika zinazoendelea kunyesha.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Divisheni ya Elimu Kinga na Ushauri Nasaha kutoka Zanzibar Disaster Management Commission, Suleiman Kheri Suleiman, wakati akitoa mafunzo kwa Kamati ya Kitaalamu ya Kukabiliana na Maafa ya Wilaya ya Kati. Mafunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa Baraza la Manispaa Kati uliopo Dunga.
Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wajumbe wa kamati hizo ili kufahamu vyema majukumu yao pamoja na mbinu sahihi za kukabiliana na maafa, hatua itakayowasaidia kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi katika kulinda maisha na mali za wananchi.
Kwa upande wake, Kaimu OCD wa Wilaya ya Kati, Joram Namala Samson, amesema mafunzo hayo yatasaidia kuimarisha ushirikiano kati ya kamati za maafa na Polisi Jamii ili kuwafikia wananchi na kuwapatia elimu juu ya athari na namna ya kujikinga na maafa yanapotokea.
Naye Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Kati, Dk. Mwanaisha Ali Said, amesema mafunzo hayo pia yamewasaidia wajumbe kujifunza umuhimu wa maandalizi ya kifedha, ikiwemo kuweka mfuko wa akiba utakaosaidia kuwahudumia wananchi wanapokumbwa na majanga katika jamii.
Aidha, Dk. Mwanaisha amewahimiza wananchi kuondokana na dhana ya kusubiri misaada kutoka serikalini pekee, badala yake wawe na utamaduni wa kujiwekea akiba ili kukabiliana na changamoto za maafa pindi zinapotokea.
Ameongeza kuwa wajumbe wa kamati za kukabiliana na maafa Wilaya ya Kati wanapaswa kuyafanyia kazi mafunzo waliyopatiwa ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa manufaa ya jamii.