Zenj FM

TPF-Net yaleta neema ya maji kambi ya Polisi Ziwani

05/03/2026, 17:02

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar Anna Atanas Poul,akizindua mradi maalum wa maji katika Kambi ya Polisi Ziwani, Zanzibar,

Na Denis Mtamwega.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar Anna Atanas Poul, amezindua rasmi mradi maalum wa maji katika Kambi ya Polisi Ziwani, Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Mtandao wa Polisi Wanawake (TPF-Net).

Uzinduzi huo unalenga kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa askari wa Jeshi la Polisi pamoja na familia zao wanaoishi katika kambi hiyo, huku  ukichangia kuimarisha ustawi wa jamii inayowazunguka.

Akizungumza mara baada ya kuzindua mradi huo, Anna amesema Serikali inaendelea kuweka mkazo katika kuboresha huduma za msingi kwa watumishi wa umma, ikiwemo askari wa vyombo vya ulinzi na usalama, ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Amesema mradi huo wa maji utasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji katika kambi hiyo na kuleta mazingira bora ya maisha kwa askari na familia zao.

Baada ya uzinduzi huo, alipata fursa ya kuzungumza na askari wa kike pamoja na wakazi raia katika ukumbi wa Chuo cha Polisi Zanzibar, ambapo aliwahamasisha wanawake kuendelea kuwa na mshikamano, kufanya kazi kwa bidii na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

Aidha, amewataka askari wanawake kuendelea kuwa mfano wa uadilifu, uwajibikaji na nidhamu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kulinda usalama wa raia na mali zao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake Zanzibar ambae ni Mrakibu mwandamizi wa Polisi (SSP) Pili Fobbe amemshukuru na kumpongeza Waziri pamoja na wadau mbalimbali waliofanikisha mradi huo, akieleza kuwa mradi wa maji utakuwa na manufaa makubwa kwa askari pamoja na wananchi wanaozunguka kambi hiyo.

Maadhimisho ya Mtandao wa Polisi Wanawake (TPF-Net) yanafanyika kwa lengo la kuimarisha ushiriki wa wanawake ndani ya Jeshi la Polisi pamoja na kuhamasisha maendeleo ya kijamii na ustawi wa familia.