Zenj FM
Zenj FM
28/02/2026, 16:11

Na Mary Julius.
Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imetangaza rasmi kukamilisha zoezi la kuteketeza nyaraka za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kwa mujibu wa matakwa ya Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2018.
Akizungumza katika zoezi hilo lililofanyika kijiji cha Muyuni, Mwenyekiti wa Tume, George Joseph Kazi, amesema kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2018, Tume inapaswa kuteketeza nyaraka za uchaguzi siku 90 baada ya Uchaguzi Mkuu iwapo hakuna amri ya mahakama inayozuia zoezi hilo.
Amebainisha kuwa zoezi hilo lilianza katika kisiwa cha Pemba baada ya kuthibitika kuwa hakukuwa na zuio lolote la kimahakama.
Ameongeza kuwa Tume inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, na mtu yeyote anayeona kuwa kuna ukiukwaji wa sheria ana haki ya kufungua shauri mahakamani ili kupata tafsiri sahihi ya kisheria.
Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Tathmini na Uhamishaji Nyaraka kutoka Taasisi ya Nyaraka, Zuwena Rajab Ali, amesema kwa mujibu wa Sheria ya Nyaraka ya mwaka 2008 (kifungu cha 13 hadi 15), taasisi hiyo ina jukumu la kusimamia zoezi la uteketezaji wa nyaraka za umma.
Amefafanua kuwa taasisi yao haihifadhi karatasi za kura kwa matumizi ya baadaye, bali huhifadhi matokeo rasmi ya uchaguzi kama kumbukumbu ya kudumu.
Naye Sheha wa Muugoni, Mussa Juma Mbwato, amesema serikali ya kijiji ilipokea taarifa ya kufanyika kwa zoezi hilo na kuliridhia, na kwamba lilifanyika kwa amani na usalama.