Zenj FM
Zenj FM
25 February 2026, 1:06 am

Na Mary Julius.
Taasisi za wasaidizi wa kisheria nchini zimeendelea kuwa nguzo muhimu katika kusogeza huduma za haki karibu na wananchi, hasa wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za mawakili na wanasheria binafsi.
Hayo yameelezwa na Afisa Miradi wa Mwavuli wa Jumuiya za Wasaidizi wa Kisheria Zanzibar (ZAPONET), Almas Muhammed, wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha wawakilishi wa taasisi hizo kilichofanyika katika ofisi za ZAPONET, Kikwajuni, Mjini Unguja.
Almas amesema kabla ya kuimarika kwa mtandao wa wasaidizi wa kisheria, wananchi wengi walishindwa kudai haki zao kutokana na ukosefu wa msaada wa kisheria na uelewa mdogo wa sheria.
Amebainisha kuwa kwa sasa huduma hizo zimekuwa tegemeo kwa watu wa kipato cha chini wanaokumbana na changamoto za migogoro ya ardhi, ajira, ndoa na talaka, pamoja na masuala ya unyanyasaji, ukatili wa kijinsia na udhalilishaji.
Aidha, amesema kikao hicho ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya mwavuli huo baada ya kubaini baadhi ya taasisi kukosa nyenzo muhimu za kiutawala kama miongozo ya fedha na rasilimali watu, hali inayochangia kushindwa kuvutia ufadhili na kujiendesha kwa ufanisi.
Akifungua kikao hicho, Mkurugenzi wa ZAPONET, Asia Abdisalam Hussein, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo watendaji wa taasisi hizo katika usimamizi wa fedha, rasilimali watu na uratibu wa shughuli zao za kila siku.
Amesema lengo ni kuhakikisha kila taasisi inakuwa na sera na kanuni zinazoendana na mahitaji ya sasa, ili kuimarisha uwajibikaji, kuongeza ufanisi na kuweka msingi imara wa taasisi endelevu.
Kwa upande wake, Ofisa Programu kutoka Legal Services Facility (LSF), Bakar Hamad, amewataka washiriki kuwa na mikakati thabiti ya kutafuta na kusimamia miradi kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali na mwelekeo wa kimataifa, ili kujijengea ushindani katika soko la ufadhili.
Nao Baadhi ya washiriki wa kikao hicho, akiwemo Mkurugenzi wa Shirika la Msaada wa Sheria Wilaya ya Kaskazini A (NAPAC), Asia Fadhil Makame, amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka ambapo jamii imeanza kutambua mchango wa wasaidizi wa kisheria katika upatikanaji wa haki na utatuzi wa migogoro.
Kikao hicho cha siku mbili kiliwakutanisha wahasibu na wakurugenzi wa taasisi za wasaidizi wa kisheria kutoka wilaya zote za Unguja, huku kikao kama hicho kikifanyika pia Pemba, kwa lengo la kuimarisha utendaji, kuongeza uwajibikaji na kujenga taasisi zenye misingi imara ya kisheria na kiutawala.