Zenj FM

Wanawake wenye ulemavu wainua sauti,saini itifaki ya Afrika

30 January 2026, 11:23 am

Afisa Utetezi na Uchawishi Katika Kikundi Cha WUKU Mwema Ali Ameir akiwa na wanachama wa kikundi cha wanawake wenye ulemavu Kusini unguja.

Na Mary Julius.

Wanachama wa vikundi vya wanawake wenye ulemavu Kusini Unguja WUKU wametakiwa kutumia ipasavyo mafunzo waliyoyapata kupitia mradi wa kuwezesha utetezi wa haki za wanawake wenye ulemavu, na kuunga mkono kusainiwa kwa itifaki ya afrika kuhusu  haki za watu wenye ulemavu  ili kujiongezea kipato na kujiendeleza kiuchumi.

Wito huo umetolewa na Kiongozi wa Programu wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (UWZ), Dolnad Godwin Navetta wakati wa kikao cha mwisho cha tathmini na kupokea mrejesho wa utekelezaji wa mradi huo, kilichofanyika katika ofisi za UWZ, Kikwajuni, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesema iwapo wanawake hao watayatumia kikamilifu mafunzo waliyopatiwa, vikundi vingi vitaondokana na utegemezi wa kiuchumi na kuimarisha uwezo wao wa kujitegemea.

Sauti ya Programu wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (UWZ), Dolnad Godwin Navetta.

Kwa upande wake, Afisa Utetezi na Uchawishi Katika Kikundi Cha WUKU Mwema Ali Ameir, amesema katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi huo, wamefanikiwa kutoa mafunzo kwa makundi mbalimbali yakiwemo vikundi vya watu wenye ulemavu, waandishi wa habari, pamoja na kufanya mikutano na maafisa wa serikali, iliyowakutanisha Wakurugenzi na Makatibu Wakuu kutoka wizara na taasisi tofauti za serikali.

Ameeleza kuwa lengo la mikutano hiyo lilikuwa ni kuielimisha jamii kuhusu Itifaki ya Afrika ya haki za watu wenye ulemavu, pamoja na kuimarisha utetezi wa itifaki hiyo kwa kuwashirikisha wanawake wenye ulemavu katika mchakato huo.

Sauti ya Afisa Utetezi na Uchawishi Katika Kikundi Cha WUKU Mwema Ali Ameir,

Nao wanufaika wa mradi huo wamesema kuwa licha ya mradi kufikia tamati, wataendelea kutumia maarifa waliyoyapata kutoa elimu kwa watu wenye ulemavu na jamii kwa ujumla, ili kujikwamua kiuchumi na kijamii.

Aidha, wameiomba Serikali kusaini Itifaki ya Afrika kuhusu haki za watu wenye ulemavu, wakisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha upatikanaji wa haki za msingi na kuongeza ujumuishi wa watu wenye ulemavu katika jamii.