Zenj FM

Sekta binafsi yahimizwa kusaidia kuokoa maisha kupitia uchangiaji damu

27 January 2026, 2:46 pm

Daktari Dhamamana wa Upasuaji katika Hospitali ya Jitimai, Dk. Shabbier Adam akichangia damu katika kambi ya hospital ya Jitimai Magogoni Zanzibar.

Na Mary Julius.

Balozi wa Utalii Zanzibar, Lois Inninger, amezitaka kampuni binafsi zinazofanya shughuli zake hapa nchini kurudisha kwa jamii sehemu ya faida wanazozipata, kwa kuchangia misaada mbalimbali itakayosaidia kuboresha ustawi wa jamii, hususan katika sekta ya afya.

 Balozi Inninger ameyasema hayo  alipokuwa akizungumza katika kambi ya uchangiaji damu iliyoandaliwa na Hospitali ya Seifii, iliyofanyika katika hospital mbili ya Mbuzini na Jitimai ambapo amesisitiza kuwa upatikanaji wa damu ni jambo muhimu sana katika kuboresha huduma za afya na kuokoa maisha ya binadamu.

Amebainisha kuwa licha ya kujihusisha na shughuli za utalii, ameona umuhimu wa kushiriki moja kwa moja katika masuala ya afya kwa kuwa kuchangia damu ni njia ya haraka na yenye mchango mkubwa katika kuokoa maisha (save lives).

Sauti ya Balozi wa Utalii Zanzibar, Lois Inninger.

Kwa upande wake, Daktari Dhamamana wa Upasuaji katika Hospitali ya Jitimai, Dk. Shabbier Adam, amesema hospitali hiyo imefarijika sana kushiriki katika kambi hiyo ya uchangiaji damu.

Ameeleza kuwa mafanikio ya zoezi hilo yametokana na udhamini na ushirikiano wa waandaaji, hali iliyosaidia kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi.

Dk. Adam ameendelea kuitaka jamii kuendeleza utamaduni wa kuchangia damu mara kwa mara, akisisitiza kuwa damu ni nyenzo muhimu katika kuimarisha huduma za afya na kuokoa wagonjwa wengi wanaohitaji matibabu ya dharura na upasuaji.

Sauti ya Daktari Dhamamana wa Upasuaji katika Hospitali ya Jitimai, Dk. Shabbier Adam,

Naye Dk. Shadya Hassan Mohammed amewashukuru waandaaji wa kambi hiyo, akisema zoezi hilo limechangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa damu itakayotumika katika operesheni zinazotarajiwa kufanyika katika Hospitali ya Kitogani, Zanzibar.

Amefafanua kuwa kuanzia tarehe 4 hadi 7, kutafanyika kambi maalumu ya upasuaji wa bure kwa wananchi wenye matatizo sugu ya kiafya, ambapo operesheni za aina mbalimbali zitatekelezwa.

Amesema Hospitali ya Seifii imeandaa kambi hiyo kwa lengo la kusaidia jamii bila gharama yoyote.

Sauti ya Dk. Shadya Hassan Mohammed.

Kwa upande wake, William Jeofry, mmoja wa wachangiaji damu, ametoa wito kwa Watanzania wote wenye sifa ya kuchangia damu kujitokeza kushiriki katika zoezi hilo.

Amesema kuwa kuchangia damu ni tendo la kizalendo na la kibinadamu, kwani mfadhili mmoja anaweza kusaidia kuokoa maisha ya watu wengi kwa wakati mmoja.

Sauti ya William Jeofry, mmoja wa wachangiaji damu.

Zoezi la uchangiaji damu kwa ajili ya operation inayotarajiwa kufanyika feb 4 mpaka 7 limefanyika katika hospital mbili ambazo ni jitimai na mbuzini likiwa limedhaminiwa na hospital ya seifii pamoja na Project RISE – Dawoodi Bohra Initiative.