Zenj FM

ZEC yasisitiza ushirikiano na uwazi ulivyoimarisha uchaguzi mkuu 2025

20 November 2025, 7:23 pm

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC, George Joseph Kazi Akifungua mkutano wa tathmini ya wadau uliofanyika katika ukumbi wa Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud.

Mary Julius Kitipwi.

Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imesisitiza kuwa ushirikiano mpana kati ya Tume na wadau wa uchaguzi umechangia kuendesha Uchaguzi Mkuu wa 2025 kwa uwazi, weledi na kwa kuzingatia misingi ya amani.

Akifungua mkutano wa tathmini ya wadau uliofanyika katika ukumbi wa Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC, George Joseph Kazi, amesema mafanikio yaliyopatikana ni uthibitisho kuwa uchaguzi ni jukumu la pamoja, sio la Tume pekee.

Mwenyekiti Kazi amewapongeza wadau wote kwa kuenzi kaulimbiu “Kura haki yako, amani wajibu wako”, ambayo imeongeza mwitikio wa wananchi kushiriki kwa haki na utulivu.

Amesema kuongezeka kwa uwazi katika taratibu za upigaji na kuhesabu kura, mafunzo kwa wasimamizi, elimu ya mpiga kura na kuanzishwa kwa kituo cha huduma kwa wateja kumeimarisha imani ya wananchi katika mfumo wa uchaguzi.

Amesema mafanikio hayo yamechochewa na mahusiano mazuri kati ya ZEC, vyama vya siasa, vyombo vya habari na taasisi nyingine, na ni msingi muhimu kuelekea chaguzi bora zaidi siku zijazo.

Sauti ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC, George Joseph Kazi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Thabit Idarous Faina, amesema mkutano huo unalenga kukusanya maoni ya wadau kuhusu maeneo yenye changamoto ili kuyafanyia kazi katika maandalizi ya uchaguzi wa 2030.

Wadau wa uchaguzi wameipongeza ZEC na vyombo vya ulinzi kwa kuhakikisha mazingira salama, pamoja na kuweka utaratibu uliowawezesha watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu.

Wameishauri Tume kuongeza wakalimani katika vituo vya kupigia kura ili kuimarisha zaidi ujumuishi.

Sauti ya Wadau.

Mkutano huo wa siku moja ulihudhuriwa na wakuu wa mikoa na wilaya, vyama vya siasa, SMZ, kamati ya amani ya kitaifa, waangalizi wa uchaguzi, asasi za kiraia, waandishi wa habari, Jeshi la Polisi na watendaji wa ZEC.