Zenj FM
Zenj FM
28 October 2025, 3:58 pm

Na Mary Julius.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), jaji George Joseph Kazi, amesema upigaji wa kura ya mapema umeanza vizuri, kwa wakati, na kwa hali ya amani na utulivu, huku wenye sifa ya kupiga kura hiyo wakijitokeza kutekeleza haki yao ya kikatiba ya kupiga kura.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati alipofanya ziara katika baadhi ya vituo vya kupiga kura , Mwenyekiti amesema kuwa Tume imeridhishwa na mwenendo wa zoezi hilo, ambapo baadhi ya vituo alivyotembelea vilionyesha mwitikio mzuri wa wapiga kura na maandalizi mazuri ya watendaji.
Amefafanua kuwa wapiga kura wenye sifa waliopaswa kushiriki kura ya mapema lakini hawakupata fursa leo, wataruhusiwa kupiga kura kesho endapo watapata nafasi.
Aidha Mwenyekiti ametoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi siku ya tarehe 29 Oktoba 2025, ili kutimiza haki yao ya msingi ya kupiga kura kwa amani na kudumisha utulivu wa nchi.
Mgombea udiwani wa Wadi ya Urusi Jimbo la Jangombe kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Is-Haka Saidi Hussein, amesema hali ya ulinzi na usalama katika maeneo yote ni shwari, na wananchi wanaendelea na shughuli zao kwa utulivu.
Amewataka wananchi wote kuendelea kudumisha amani na mshikamano katika kipindi chote cha uchaguzi.
Kura ya mapema imefanyika katika vituo 50 vya kupigia kura, ambapo kila jimbo lina kituo kimoja. Washiriki wakuu wa kura hiyo ni wasimamizi wa uchaguzi, watendaji wa Tume, na vikosi vya ulinzi na usalama, ambao siku ya uchaguzi mkuu watakuwa na majukumu maalum ya kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unafanyika kwa amani, uwazi na uadilifu.